• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Mamia wahama Kerio mashambulio yakizidi

Mamia wahama Kerio mashambulio yakizidi

FRED KIBOR Na STANLEY KIMUGE

MAMIA ya familia zinatoroka kutoka Bonde la Kerio kutafuta hifadhi katika miteremko ya Elgeyo, kutokana na kudorora kwa hali ya usalama katika eneo hilo.

Haya yanajiri baada ya shambulio lililotokea Jumapili katika eneo la Koitilial, Marakwet Magharibi, ambapo watu wawili waliuawa huku wengine sita wakijeruhiwa.

Watu wawili kati ya sita waliojeruhiwa wamelazwa katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH) na Eldoret Hospital mtawalia, baada ya risasi kupenyeza katika vichwa na tumboni.

Afisa Mkuu Mtendaji wa MTRH, Dkt Wilson Aruasa, alisema Jumatatu kwamba mmoja wa manusura wa shambulio hilo anatibiwa katika hospitali hiyo na yuko katika hali nzuri.

Manusura wengine wanne wanapokea matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Iten.

Taifa Leo imebaini kuwa mamia ya watu wanatoroka kutoka eneo hilo kwa wingi, wakihofia mashambulio zaidi kutokea.

Wengi wameamua kutafuta hifadhi katika mapango hatari kwenye miteremko hiyo, hata baada ya serikali kutangaza kuwatuma maafisa zaidi wa usalama ili kuimarisha doria.

Kwa upande mwingine, viongozi wanailaumu serikali kwa kutochukua hatua za kutosha, huku watu wakiendelea kuuawa kwa kiwango cha kuhofisha.

Bw Leonard Yano, ambaye ni mkazi, alisema kuwa eneo hilo limegeuka kuwa mahame, kwani watu wengi wameondoka kutoka makazi yao.

“Watu wengi wameachwa bila makao tangu mashambulio hayo kuanza mwaka 2021. Hata hivyo, shambulio la Jumapili lilizua wasiwasi zaidi miongoni mwa wenyeji. Mashambulio hayo yamekuwa yakiongezeka kila kuchao licha ya watu wengi kutokuwa na mifugo,” akasema.

Alisema kuwa miteremko hiyo ndiko mahali pekee ambapo wenyeji wanaweza kutafuta hifadhi kwani wavamizi hao hawawezi kupanda milima bila kugundulika.

“Kuna nyoka hatari katika miteremko hiyo. Watoto na wazee wanateseka sana kutokana na hali ya baridi. Tunaiomba serikali irejeshe hali ya utulivu angalau kuwawezesha watu kulala kwenye makazi yao,” akasema.

Bi Mary Kanda alisema kuwa wanakabiliwa na njaa kwani hakuna chakula chochote kwenye miteremko hiyo.

“Tunaumia sana. Tutapata afueni tu baada ya serikali kurejesha hali ya kawaida. Sisi si Wakenya tusio na hadhi. Tunataka kufurahia haki zetu sawa na wananchi wale wengine,” akasema.

Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Marakwet Magharibi, Bw Mathias Chisiambo, alisema kuwa ijapokuwa vikosi vya usalama vimewekwa katika hali ya tahadhari, watu wanahofia mashambulio zaidi kutokea.

Mbunge wa eneo hilo William Kisang ameirai serikali kuchukua hatua za haraka ili kukomesha mahangaiko wanayopitia wenyeji wa bonde la Kerio.

  • Tags

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Huenda sakata za Kemsa zitanyima Kenya...

Arsenal kuzidisha mshahara wa Saka mara nne

T L