• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
Arsenal kuzidisha mshahara wa Saka mara nne

Arsenal kuzidisha mshahara wa Saka mara nne

Na MASHIRIKA

ARSENAL wamefichua mpango wa kuzidisha mshahara wa kiungo mvamizi Bukayo Saka mara nne ili uwiane na ukubwa wa hadhi na mchango wake muhimu kambini mwa kikosi hicho.

Saka, 20, kwa sasa anadumishwa na Arsenal kwa mshahara wa Sh4.7 milioni kwa wiki uwanjani Emirates. Ujira huo unamfanya kuwa miongoni mwa wanasoka wanaolipwa mshahara wa chini zaidi katika kikosi hicho kinachotiwa makali na kocha Mikel Arteta.

Kwa mujibu wa Arteta, Arsenal wanajiandaa kumpa Saka mkataba mpya utakaomshuhudia akitia mfukoni Sh19.5 milioni kwa wiki na kuzima kabisa tetesi nyingi zinazomhusisha nyota huyo raia wa Uingereza na uwezekano wa kubanduka ugani Emirates.

“Ni miongoni mwa wachezaji bora kwa sasa kambini mwetu. Umuhimu wake umekuwa ukidhihirika katika kila mchuano. Ni wajibu wetu kumpa ofa itakayompa motisha zaidi,” akasema Arteta.

Saka angali na miaka miwili zaidi kwenye mkataba wake wa sasa na Arsenal. Alitia saini kandarasi hiyo miezi 20 iliyopita.

Licha ya kupata jeraha la mguu wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyowakutanisha na Aston Villa mnamo Machi 19, 2022, Saka anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi kitakachotegemewa na kocha Gareth Southgate wa Uingereza katika michuano ijayo ya kimataifa.

Arsenal wanatarajiwa kumfanya Saka kuwa miongoni mwa wachezaji wanaodumishwa kwa mishahara minono baada ya kupunguza gharama yao ya matumizi tangu waagane na wanasoka Mesut Ozil, Pierre-Emerick Aubameyang, Willian Borges na David Luiz.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Mamia wahama Kerio mashambulio yakizidi

Khaniri awarai Waluhya wamuunge mkono Raila

T L