• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Mandonga afunguka kuhusu kuacha ngumi baada ya kutandikwa tena Zanzibar

Mandonga afunguka kuhusu kuacha ngumi baada ya kutandikwa tena Zanzibar

Na CECIL ODONGO

Bondia maarufu Tanzania Karim Mandonga maarufu kama ‘Mandonga Mtu Kazi’ ameashiria kuwa huenda akastaafu  baada ya kuchapwa na Mula Jr  kwenye pigano la masumbwi  lililoshuhudiwa na Rais wa Zanzibar  Hassan Mwinyi Agosti 28.

Licha ya mdomo wake mwingi na kujishauashaua kuwa angepata ushindi, Mandonga, 44,  alipigwa hadi akasalimu amri katika raundi ya sita.  Kabla ya pigano hilo, Mandonga aliahidi kuwa iwapo angepigwa na  Mula Jr na pigano hilo lipite raundi ya pili  basi angestaafu ndondi moja kwa moja.

Ingawa hivyo, alikataa kutii ahadi yake kuwa angeachana na ndondi ila akatoa kauli iliyoashiria kuwa atakuwa akivumisha brandi yake ya ubondia badala ya kumakinikia pigano sana.

“Siwezi kuomba msamaha kwa kupigwa wakati ambapo mimi ndiye Mfalme wa ngumi duniani. Siwezi kufuta kauli yangu . Nilisema.  Kusema na kufanya inawezekana?  Ni brandi yangu na kwa sababu ya Mandonga ngumi imefika Zanzibari,” akasema Mandonga.

“Leo nimekuwa balozi mkubwa na nitakuwa nalipwa bilioni mbili kwa mwezi.  Watu wote unawaona ni wazima wameacha shughuli zao kuja kuona ngumi. Mtoto ni nani hapo?  Wewe uliza swali la msingi,” Mandonga akaambia mmoja wa maripota ambaye alikuwa akisisitiza kuwa aseme iwapo atastaafu au hatastaafu.

Katika kile kinachosisitiza huenda hana muda mwingi ulingoni, hotuba ya Mandonga iligusia sana ubalozi akisema mchezo huo sasa unashabikiwa sana Tanzania, Zanzibar na hata mataifa mengine kutokana na juhudi zake.

Baada ya mapigano hayo, Mandoga alisema kuwa kipigo hicho kilikuwa cha polepole akidai aliachilia raundi ya sita ilhali huwa haachi pigano mpake afike raundi ya nane au 12. Alisema alifanya hivyo, ili Rais Mwinyi asipige ngumi marufuku Zanzibar iwapo mpinzani wake angekufa au kupasuka kichwa kutokana na uzito wa ngumi zake.

Mula Jr alithibitisha kuwa Mandonga kwa kweli ni bondia na yeyote anayepigana naye lazima atumie hekima ili kumpiku.

“Huyu mzee ana nguvu na anayepigana naye ajipange na awe mjanja. Ikiwa hutembei au haupo vizuri kwenye ‘guard’ atakuvunjavunja,” akasema Mula Jr.

Mandoga amekuwa akipoteza mapigano anayoshiriki ishara kuwa huenda analemewa ulingoni. Mnamo Juni 23, alipoteza kwa Mkenya Daniel Wanyonyi katika raundi ya 10 kutokana na uamuzi wa majaji watatu.

Mnamo Julai 30 alichapwa na Bondia wa Uganda Moses Golola nyumbani Mwanza. Alipoteza pigano hilo kwenye raundi ya tatu baada ya kuangushiwa magumi mazito na Golola.

  • Tags

You can share this post!

Mapato ya wafanyakazi kuendelea kunyofolewa

Umaarufu wa Raila na Azimio eneo la Maa wafifia, wa Ruto...

T L