• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:07 PM
Umaarufu wa Raila na Azimio eneo la Maa wafifia, wa Ruto ukipanda

Umaarufu wa Raila na Azimio eneo la Maa wafifia, wa Ruto ukipanda

ROBERT KIPLAGAT na CHARLES WASONGA

MUUNGANO wa Kenya Kwanza wake Rais William Ruto unaonekana kupenya katika eneo la Maa ambalo hapo awali ulisawiriwa kuwa ngome ya chama cha ODM, chake Raila Odinga.

Hii, wadadisi wanasema, inatokana na ziara kadha ambazo Dkt Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua katika eneo hilo wakitoa “minofu” kwa lengo la kuvutia uungwaji mkono kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Takwimu zinaonyesha kuwa tangu 2007 Bw Odinga amekuwa akishabikiwa kwa kiwango kikubwa katika kaunti za Narok, Kajiado, Samburu na Laikipia, kura nyingi za urais zikiingia kapuni mwake.

Lakini hali inaonekana kubadilika kwani,  Bw Odinga anaonekana kupoteza ushawishi katika kaunti hizo za Maa.

Hii ni kutokana na kampeni kali zinazoendeshwa na Rais Ruto kupitia ziara za “kimaendeleo”, lakini yenye malengo ya kisiasa.

Majuma mawili yaliyopita, kiongozi wa taifa alipokelewa na magavana Patrick Ole Ntutu (Narok), Lati Lelelit (Samburu) na mwenzao wa Kajiado Joseph Ole Lenku alipohudhuria sherehe za kitamadunu ya jamii ya Maa kuwasilisha ujumbe mzuri kwao.

Wakati wa sherehe hizo zilizofanyika katika eneo la Sekenani Gate ndani ya mbuga ya Maasai Mara, Dkt Ruto alitangaza kuwa Mbuga ya Kitaifa ya Amboseli itasimamiwa na serikali ya Kaunti ya Kajiado.

Tangazo hilo lilimfanya Gavana Lenku kutokwa na machozi ya furaha.

Rais alifafanua kuwa kaunti ambako kunapatikana mbuga za kitaifa zitagawana mapato kutoka rasilimali hizo na serikali ya kitaifa nusu bin nusu.

Hii inaashiria kuwa kaunti tatu za Maa zitafaidi kwa kuwa na mbuga kubwa za wanyamapori nchini.

Hizo ni Mbuga ya Kitaifa ya Maasai Mara (iliyoko kaunti ya Narok), Amboseli (Kajiado) na Mbuga ya Kitaifa ya Samburu iliyoko Kaunti ya Samburu.

Katika Kaunti ya Narok, Rais Ruto pia aliahidi kuwa serikali yake itajenga kiwanda cha maziwa kitakachomilikiwa na kampuni ya maziwa ya New KCC, eneo la kiviwanda na kichinjio cha kisasa kuongeza thamani kwa bidhaa za mifugo.

“Hii ni serikali yenu. Hamna serikali nyingine. Licha ya kwamba nyakati zingine huwa mwaenda kinyume nami nikitaka kura zetu, nawapenda na ningetaka kufanya kazi nanyi,” Rais Ruto akawahakikishia viongozi na watu wa jamii ya Maa.

Gavana Ole Lenku ambaye ni msemaji wa jamii ya Maasai na mwenyekiti wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Narok-Kajiado (NAKAEB) ameapa kufanya kazi na utawala wa Ruto licha ya kwanma alichaguliwa kwa tiketi ya ODM.

“Tunamshukuru Rais kwa kurejesha mbuga ya Amboseli kwa watu wa Kajiado. Imekuwa ni safari ndefu yenye changamoto nyingi. Kwa sababu hii sisi kama jamii ya Maa tunaunga mkono utawala wako kwa manufaa ya watu wetu,” akasema Bw Lenku.

Pigo jingine kwa Bw Odinga, chama cha ODM na muungano wa Azimio lilidhihirika Jumatatu baada ya mwenyekiti wa chama hicho cha Chungwa katika eneo bunge la Narok Kaskazini Bw Maranka Ole Otuni kujiunga na mrengo wa Kenya Kwanza.

Akipokelewa na Gavana Ntutu, Bw Otuni alisema kuwa jamii ya Maa imekuwa kwenye “baridi” kwa muda mrefu na sasa “tunafaa kufurahia keki ya kitaifa.”

Kiongozi mwingine ambaye anafanya kazi na serikali ya Kenya Kwanza ni Mbunge wa Kajiado ya Kati Memusi Kanchori.

Bw Kanchori amechaguliwa kwa mihula miwili, kuwakilisha eneo bunge hilo bungeni, kwa tiketi ya ODM.

Kwa mara ya kwanza katika Kaunti ya Narok, kando na Seneta Ledama Ole Kina, chama cha ODM hakina mbunge katika maeneo bunge yote sita.

Lakini licha ya kukosa wabunge, katika uchaguzi wa urais wa 2022, Bw Odinga alimshinda Ruto katika kaunti hii, sawa na kaunti za Kajiado na Samburu.

Kwa mfano katika kaunti ya Narok, Odinga alizoa jumla ya kura 159,455 (sawa na asilimia 51 za kura zote zilizopigwa huku Dkt Ruto akipata kura 148,310 (asilimia 48).

Katika Kaunti ya Samburu Odinga alipata kura 41, 737 (sawa na asilimia 59) huku Dkt Ruto akipata kura 28,329.

Hali ilikuwa ni hivyo katika Kaunti ya Kajiado ambapo Odinga aliibuka kidedea kwa kuzoa kuwa 158,556 huku Dkt Ruto akipata kura 148,497.

  • Tags

You can share this post!

Mandonga afunguka kuhusu kuacha ngumi baada ya kutandikwa...

TUONGEE KIUME: Kutuma nauli na utapeli mwingine wa baadhi...

T L