• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Mapato ya wafanyakazi kuendelea kunyofolewa

Mapato ya wafanyakazi kuendelea kunyofolewa

CECIL ODONGO na RICHARD MUNGUTI

WAKENYA, hasa wafanyakazi wanatarajiwa kuendelea kufyonzwa zaidi kufuatia kuwasilishwa bungeni kwa mswada unaopendekeza wafanyakazi kuchangia hazina ya kuwakimu wale ambao wamepoteza ajira.

Mswada wa Kubuniwa kwa Mamlaka ya Kuwakimu Wasio na Ajira, 2023 (UIA, Bill) ambao umedhaminiwa na Mbunge wa Ikolomani, Benard Shinali pia unalenga kuwanusuru jamaa za waliopoteza ajira.

Watu ambao wameajiriwa katika sekta za umma na ile ya kibinafsi ndio watakuwa wakichangia Hazina hiyo kwa pesa ambazo zitakatwa kutoka kwa mishahara yao kila mwezi.

Hii bila shaka itawaongezea wafanyakazi hao mzigo zaidi ikizingatiwa kuwa wanazongwa na mzigo waliotwikwa na Sheria ya Fedha, 2023 iliyopendekeza ushuru mpya wa nyumba na nyongeza za aina mbalimbali za ushuru.

Ushuru wa nyumba wa kima cha asilimia 1.5 ya jumla ya mapato tayari imenza kutekelezwa licha ya kesi inayoendelea mahakamani.

Jana, Mahakama ya Juu ilitupilia mbali kesi iliyowasilishwa na Seneta wa Busia, Okiya Omtata aliyetaka utekelezaji wa ushuru huu usimamishwe hadi kesi aliyoiwasilisha katika Mahakama Kuu isikizwe na kuamuliwa. Hii ina maana wafanyakazi wataendelea kuumia.

Aidha, serikali imependekeza kuongeza mchango wao kwa hazina mpya ya afya ya kijamii (SHIF) hadi asilimia 2.75. Hazina hii itachukua mahala pa ile ya sasa ya NHIF.

Isitoshe, Rais William Ruto ameamuru mchango wa wafanyakazi kwa Hazina ya Kitaifa ya Malipo ya Uzeeni (NSSF) uongezwa kutoka Sh200 hadi Sh2000 kila mwezi.

Alipofika mbele ya Kamati ya Bajeti mnamo Alhamisi, Bw Shinali alisema mswada wake una nia njema kwa sababu mpango kama huo wa kuwakimu waliopoteza ajira unatekelezwa nchi zingine ikiwemo Afrika Kusini.

“Lengo la hazina hii ni kuhakikisha wale ambao wameajiriwa na wakapoteza kazi wanaendelea kunufaika pamoja na familia zao au wale ambao walikuwa wakiwategemea. Hii ndio njia ya kuwakwamua kutoka hali ngumu ya maisha baada ya kupoteza ajira,” akasema Bw Shinali.
Kando na mwajiri na mwajiriwa, pesa za hazina hii zitakuwa pia zikitolewa kwenye sehemu ya bajeti, pesa za kaunti na pia michango na hisani kutoka mashirika na watu mbalimbali.

Pia mbunge huyo wa ODM anapendekeza kuanzishwa kwa Mamlaka ya Bima kwa Wasioajiriwa ambayo itakuwa asasi yenye bodi iliyo na mwenyekiti pamoja na wanachama tisa.

Mamlaka hiyo itakuwa ikifuatilia matumizi ya pesa ya hazina na kumshauri Waziri wa Leba kuhusu sera ya bima kwa wasioajiriwa pamoja na sheria.

Mswada wa Bw Shinali pia unatoa mwanya wa kuteuliwa kwa wafanyakazi wa mamlaka hiyo ili itekeleze kazi yake ipasavyo na kwa mujibu wa sheria.

Ingawa hivyo, Waziri wa Leba ana mamlaka ya kuwateua watumishi wa umma ambao hawatatoa mchango kwa hazina kupitia ushauri wa Tume ya Kudhibiti na Kuoanisha Mishahara Nchini (SRC).

Kando na hayo, Wakenya wanaofanya kazi ng’ambo nao wanatarajiwa kukatwa pesa zitakazoelekezwa kwenye hazina ya kuwafaa wenzao wanaokumbwa na shida wakiwa ughaibuni.

Makato hayo ya lazima yataelekezwa kwenye Hazina Maalum Wafanyakazi wa Nje ya Nchi.

  • Tags

You can share this post!

Dereva wa teksi aliyekula Sh40,000 za karao ajutia kitendo...

Mandonga afunguka kuhusu kuacha ngumi baada ya kutandikwa...

T L