• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Manusura wa jengo lililoporomoka aaga dunia

Manusura wa jengo lililoporomoka aaga dunia

Na SIMON CIURI

MMOJA kati ya walionusurika Jumatano baada ya nyumba ya ghorofa kuanguka eneo la Gachie, Kaunti ya Kiambu, amekufa. Mwanaume huyo aliyekuwa mmoja wa wajenzi katika ghorofa hiyo alikufa kutokana na majeraha aliyopata.

Afisa mkuu wa shirika la zima moto wa kaunti hiyo, Samuel Kahura, aliambia Taifa Leo kuwa mwathiriwa huyo alikufa jana asubuhi akipokea matibabu katika hospitali ya Tigoni.

“Kwa bahati mbaya tumempoteza mmoja kati ya watu tisa waliookolewa jana. Alikufa kutokana na majeraha aliyopata,” akasema Bw Kahura.

Shirika la Msalaba Mwekundu na mashirika ya kutoa msaada wa dharura kutoka kaunti za Kiambu na Nairobi yalifika katika eneo hilo la tukio ili kuwaokoa waliokuwa wamekwama katika jengo hilo.

“Hadi sasa, hatujaweza kuwaokoa waathiriwa wengine. Hata hivyo, tunaendelea kusaka jengo hilo ili kuwaokoa wengine waliokuwa wakifanya ujenzi lilipoanguka,” Bw Kahura akaambia Taifa Leo.

Kulingana na walioshuhudia, jengo hilo lilianguka wajenzi hao wakiwa katika orofa ya tano.Kamanda wa polisi wa kaunti ya Kiambu, Ali Nuno, alisema wanamsaka mmiliki wa ghorofa hiyo ili aeleze kwa nini alikiuka amri ya serikali ya kusimamishwa kwa ujenzi wa jengo hilo.

Katika miaka ya hivi karibuni, visa vya majengo hasa ya ghorofa kuporomoka vimekuwa vikiongozeka huku wamiliki wa nyumba hizo wakidaiwa kuharakisha mafundi ili kupunguza gharama.

Isitoshe, wengi hawafuati kanuni za ujenzi wala kupokea idhini kutoka kwa asasi zinazohusika na ujenzi hasa katika sehemu za miji.

You can share this post!

Wafuasi 13 wa UDA washtakiwa kwa ukiukaji wa kanuni za...

Kitany na DCI wapinga kinga ya Linturi kortini