• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 3:07 PM
Kitany na DCI wapinga kinga ya Linturi kortini

Kitany na DCI wapinga kinga ya Linturi kortini

Na JOSEPH WANGUI

ALIYEKUWA mke wa Seneta wa Meru Mithika Linturi, Maryanne Kitany, na polisi sasa wanataka mahakama ifutilie mbali agizo la kuzuia kiongozi huyo asikamatwe kwa madai ya kujaribu kubaka mwanamke mjini Nanyuki.

Bi Kitany na polisi wanataka Bw Linturi akamatwe kuhusiana na kisa hicho kilichotokea Januari 29, mwaka huu, katika hoteli ya Maiyan Villas.

Bw Linturi, hata hivyo, amemshutumu mlalamishi pamoja na mumewe kwa kujaribu kumtoza hongo ya Sh1 milioni. Bi Kitany, Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) wanataka korti kuondoa agizo ambalo lilizuia Bw Linturi kukamatwa na polisi.

Wanasema kuwa seneta huyo alikimbia mahakamani kuomba kinga ya kutokamatwa hata kabla ya mashtaka dhidi yake kuidhinishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP).

Bw Linturi, kupitia kwa wakili wake Charles Benedict Mwongela, anataka mahakama iendelee kumkinga dhidi ya kukamatwa na polisi. Mnamo Mei 11, mwaka huu, korti ilizuia polisi kumtishia, kumkamata na kumfikisha mahakamani Bw Linturi.

“Ombi la Linturi kuzuia kukamatwa kwake na kushtakiwa linalenga kufanya kesi kujikokota,” akasema Bi Kitany.

DPP na DCI wanasema kuwa kinga hiyo inachelewesha walalamishi kupata haki na pia ni kutumia vibaya korti.Inspekta Mkuu Keith Robert Namukhasi, DCI na DPP walisema kuwa agizo lililotolewa miezi minne iliyopita la kutaka Bw Linturi asikamatwe linahusiana na mashtaka 37 yanayohusu fedha alizokopa kutoka benki ya Family na ulaghai.

“Agizo lililotolewa na mahakama hii halikukinga Linturi dhidi ya kukamatwa kwa makosa yote.“Linturi amefasiri vibaya agizo la mahakama na anadhani kwamba hawezi kuchunguzwa au kukamatwa kwa uhalifu wa aina yoyote,” akasema Inspekta Namukhasi.

DCI walisema uchunguzi dhidi ya Linturi kuhusiana na madai ya ubakaji ulianza Januari na hata yeye anafahamu kwani amewahi kuandikisha taarifa kwa polisi. Baada ya kukamilishwa kwa uchunguzi huo, faili yake ilipelekwa kwa DPP ambaye hajatoa uamuzi wowote kuhusu mwelekeo wa kesi hiyo.

“Kesi kuhusu madai ya ubakaji ni tofauti na kesi inayoendelea kortini ambapo anakabiliwa na mashtaka 37. Agizo lililotolewa asihangaishwe au kukamatwa linahusiana na kesi hiyo ya mashtaka 37. Agizo hilo halina uhusiano na madai ya ubakaji,” akasema Bw Namukhasi.

Inspekta pia alipuuzilia mbali madai ya Bw Linturi kwamba madai yanayomwandama kuhusu ubakaji yanatokana na siasa ya uchaguzi mdogo wa udiwani katika Wadi ya Kiagu, Kaunti ya Meru.

“Siasa haifai kuingizwa katika masuala ya mahakama. DCI na DPP wanatekeleza wajibu wao wa kikatiba na hawana haja na siasa za Bw Linturi,” akasema. Jaji Weldon Korir aliagiza kuwa ombi hilo litasikizwa Oktoba 12, mwaka huu.

Bw Linturi anashikilia kuwa endapo atakamatwa mkewe wa zamani Bi Kitany ambaye amemshtaki katika kesi ya ulaghai, huenda akashinda.

‘Maafisa wa DCI wakinikamata watanilazimisha kubadili msimamo wangu wa kisiasa wanasiasa wanapojipanga kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2022. Polisi wanalengaa kuninyamazisha kutokana na msimamo wangu wa kukosoa serikali,” akadai Bw Linturi.

You can share this post!

Manusura wa jengo lililoporomoka aaga dunia

Nyota wa kigeni wa Olimpiki waingia Kip Keino Classic