• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Matumaini ya kufufuka kwa Mumias yaimarika

Matumaini ya kufufuka kwa Mumias yaimarika

Na VICTOR RABALLA

HATIMAYE kuna matumaini kwenye juhudi za ufufuzi wa Kampuni ya Sukari ya Mumias, baada ya wawekezaji kupewa hadi mwishoni mwa mwezi huu kuwasilisha maombi yao ya kuwekeza kwenye kampuni hiyo.

Tangazo hilo linajiri miezi miwili baada ya kampuni za Devki kuondoa ombi lake kufuatia malalamishi kuwa utaratibu huo haukuendeshwa kwa njia ya uwazi.

Kulingana na tangazo lililochapishwa katika magazeti, wawekezaji wamepewa hadi Agosti 31, 2021 kuwasilisha maombi yao.

“Tungependa kuwaalika wale ambao wangependa kuwasilisha maombi yao kuwekeza katika kiwanda hiki ili kuimarisha utendakazi wake tena,” likaeleza tangazo.

Benki ya Kenya Commercial (KCB) ilimteua Bw Ponangipalli Venkata Ramana Rao kusimamia mchakato huo. Bw Rao alisema wanawatafuta watu ambao watawekeza na kusimamia mali yote inayomilikiwa na kampuni hiyo.

Mali hiyo inajumuisha kiwanda cha sukari, kiwanda cha kutengenezea ethanoli, kiwanda cha kutengenezea maji ya kunywa, makazi ya watu, hoteli, klabu, uwanja wa kuchezea gofu kati ya nyingine.“Tutakodisha mali hiyo kwa ada itakayokubalika na kila upande,” ikasema taarifa hiyo.

Bw Rao alisema mali hiyo ilikuwa ikitumika kuchukulia mikopo kutoka kwa mashirika mbalimbali. Alieleza mchakato wa kukodisha mali hiyo utamalizika baada ya taratibu zifaazo kukamilika.

Kampuni hiyo iliwekwa kwenye mnada mnamo Septemba 20, 2019 katika juhudi za kufufua shughuli za usagaji miwa.Ili maombi ya mwekezaji yaweze kukubaliwa, lazima ayaambatanishe na Sh25,000.

Vilevile, lazima aonyeshe jinsi atakavyoboresha usimamizi wa kituo hicho na kuimarisha hali ya maisha ya wenyeji kwa kuwapa nafasi za ajira.

“Wawekezaji watakaokodishiwa mali hiyo watapewa nafasi ya kuangalia hali yake. Watakuwa huru kuuliza maswali na kupata ufafanuzi kuihusu,” likaeleza.

Mchakato wa kufufua kampuni hiyo ulisimamishwa mnamo Juni baada ya wakulima, wafanyakazi na viongozi wa kisiasa kutoka eneo la Magharibi kumlaumu meneja aliyeteuliwa na KCB kwa kutowashirikisha wananchi.

Walidai alipanga njama kutoa kandarasi kwa Kampuni ya Devki Group, ambayo hutengeneza chuma na simiti.

Wakiongozwa na kiongozi wa ANC, Musalia Mudavadi, viongozi hao waliiomba benki hiyo kuwashirikisha wakulima kikamilifu ili kuhakikisha kiwanda hicho kimerejesha hadhi yake kama ilivyokuwa awali.

Kiwanda hicho ndicho kilikuwa kikiongoza nchini kwa kuzalisha sukari kabla ya kuanguka.Maafisa wa serikali wanasema wana imani kitarejesha hadhi yake kama ilivyokuwa awali.

You can share this post!

Kamishna atishia kufunga baa zinazokiuka kanuni za kuzuia...

Rais Suluhu, SADC waomboleza kifo cha waziri wa ulinzi wa TZ