• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
Mbunge awahimiza vijana na wafanyabiashara Ruiru kuunda makundi ili kupata mikopo ya serikali

Mbunge awahimiza vijana na wafanyabiashara Ruiru kuunda makundi ili kupata mikopo ya serikali

Na SAMMY WAWERU

MBUNGE wa Ruiru Bw Simon King’ara amewahimiza vijana na wafanyabiashara eneo hilo kuunda makundi ili kupata mikopo kujiendeleza.

Bw King’ara amesema vijana na kina mama wanapaswa kutumia fursa ya mikopo inayosambazwa na serikali kujiimarisha kimaendeleo.

Alisema hayo wakati akizungumzia wamiliki wa tuktuk eneo la Githurai 45. Akiwaahidi kuwapiga jeki, mbunge huyo aliwahimiza kutengeneza makundi ya kijamii ili waweze kuimarisha biashara yao ya usafiri na uchukuzi eneo hilo kupitia mikopo ya serikali.

“Kufikia sasa nimesambaza zaidi ya Sh75 milioni kwa makundi mbalimbali eneobunge la Ruiru. Ninawahimiza muunde makundi ili mfaidike,” akaambia wahudumu hao.

Mtaa wa Githurai 45 uko katika eneobunge la Ruiru, Kaunti ya Kiambu.

“Mhakikishe kundi mtakalotengeneza limesajiliwa chini ya Idara ya Masuala ya Jinsia Utamaduni na Huduma za Kijamii (SCDO),” akashauri.

SCDO ni idara ya serikali inayosajili makundi ya kijamii baada ya kuwasilisha ajenda, malengo, idadi ya wanachama na kumbukumbu za mikutano iliyoandaliwa ili kuyaunda.

Siku kadha zilizopita, Rais Uhuru Kenyatta aliwataka vijana kuchukua mikopo ya serikali ili waanzishe biashara na pia kujiendeleza kimaisha.

Rais Kenyatta alisema hayo baada ya kukutana na wawekezaji wachanga kutoka maeneo tofauti nchini katika Uga wa Kimataifa wa Safaricom Kasarani, jijini Nairobi.

Mikopo ya serikali inasifiwa kwa kutotozwa riba ya juu na pia wanaoichukua kupewa muda wa kutosha kurejesha pesa.

  • Tags

You can share this post!

Mfanyabiashara aliuawa kinyama – Uchunguzi

Jinsi serikali inavyozima kampeni ya wilibaro ya Ruto