• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 7:50 AM
Mchuuzi wa ndizi taabani kwa kupatikana na Sh900,000 ndani ya benki

Mchuuzi wa ndizi taabani kwa kupatikana na Sh900,000 ndani ya benki

Na RICHARD MUNGUTI

MCHUUZI wa ndizi alipatikana na hatia ya kukutwa ndani ya benki akiwa hundi ya Sh0.9milioni aliyojua imeibwa.

Kufuatia uamuzi huo Ronald Gorbachev Nyakweba aliamriwa azuiliwe rumande hadi Mei 20,2021 mahakama itakapoamua ikiwa atafungwa jela ama atapewa kifungo cha nje.

Nyakweba mwenye umri wa miaka 43, alipatwa na hatia na hakimu mwandamizi Bw Bernard Ochoi.

Akichambua ushahidi uliowasilishwa na Benki ya National (NBK), Bw Ochoi alisema mshtakiwa alikamatwa punde alipomkabidhi mfanyakazi wa benki hiyo Bi Rose Buyabo.

Muuza ndizi huyo alikuwa anasubiri kupokea maelfu ya pesa polisi walipoitwa na kuelezwa hundi ya Sh908,902 aliyokuwa nayo Gorbachev ilikuwa imeibwa kutoka benki ya Credit (CBL) mnamo Oktoba 12,2017.

Alipohojiwa na polisi mshtakiwa alikiri kwamba alipewa hundi hiyo na mwanamke, mteja wake aliyekuwa anamuuzia ndizi.

“Mshtakiwa alieleza hii mahakama akijitetea kuwa alipewa hundi hiyo apelike benki kupokea pesa hizo na mwanamke mteja wake wa kununua ndizi,” Bw Ochoi alisema akichambua ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka.

Akasema Bw Ochoi , “Ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka ulio ongozwa na wakili wa Serikali Bw James Gachoka umethibitisha mshtakiwa alipatikana na hundi ya CBL iliyokuwa imeibwa.”

Hakimu alisema upande wa mashtaka pia umethibitisha mshtakiwa alimkabidhi Bi Buyabo hundi hiyo iliyokuwa imeibwa kutoka CBL.

Lakini Bw Ochoi alitupilia mbali shtaka dhidi ya Gorbachev la kuiba hundi hiyo.

Bw Gachoka aliomba mahakama ichukulie hilo kuwa kosa la kwanza kufanywa na mshtakiwa.

“Sina rekodi za hapo awali za mshtakiwa. Naomba hii mahakama ichukulie hili kuwa kosa lake la kwanza kufanya,”alisema Bw Gachoka.

Wakili David Ayuo aliyemwakilisha mchuuzi huyo wa ndizi aliiomba mahakama msamaha pamoja na Benki za CBL na NBK .

“Mshtakiwa ameghairi matendo yake. Ameoa na wamebarikiwa na watoto watoto na pia anawatunza watoto wa nduguye aliyefariki. Naomba korti imfunge nje,”Bw Ayuo alimsihi hakimu.

Wakili huyo pia alieleza mahakama kuwa mshtakiwa yuko na ugojwa wa kisukari na kwamba anahitaji madawa kila mara.

Bw Ochoi aliagiza idara ya urekebishaji tabi imhoji mshtakiwa pamoja na watu wa familia yake kabla ya kupitishwa hukumu.

“Kabla ya kupitisha hukumu hii mahakama yahitaji ripoti ya afisa wa urekebishaji tabia ya mshtakiwa , watu wa familia zake na wahasiriwa wa uhalifu huo,” aliamuru Bw Ochoi.

Hakimu huyo aliagiza mshtakiwa azuiliwe hadi Mei 20, 2021 mahakama itakapokabidhiwa ripoti hiyo ndipo ipitishe hukumu.

You can share this post!

Sichukii wanaume, ninazingatia haki ninapotoa uamuzi...

Mwanamitindo chipukizi kuwakilisha Kenya katika mashindano...