• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Minisketi zasababisha mvutano Malindi

Minisketi zasababisha mvutano Malindi

Na CHARLES LWANGA

WADAU wa utalii mjini Malindi, Kaunti ya Kilifi wamepinga mapendekezo kuhusu marufuku ya biashara za vileo na minisketi katika bustani mpya ya Bunthwani inayotarajiwa kufunguliwa Februari.

Mwenyekiti wa Chama cha Wahudumu wa Hoteli (KAHC) eneo la Pwani Kaskazini, Bi Maureen Awuor, alisema Malindi ni mji wa kitalii ambao huvutia wageni kutoka kote ulimwenguni, na hivyo basi endapo pendekezo hilo litapitishwa litaathiri utalii.

“Malindi kama mji wa kifahari unatambulika kwa ufuo wake wa bahari na watu wakarimu. Pendekezo hilo linafaa kutupiliwa mbali kwa sababu bustani ya Bunthwani inapatikana katika ufuo wa Bahari Hindi,” alisema Bi Awuor, ambaye pia ni meneja wa hoteli ya Ocean Beach mjini humo.

Gavana wa Kilifi, Amason Kingi anatarajiwa kufunguwa rasmi bustani ya Bunthwani Hindi mwezi ujao baada ya ukarabati kukamilika kwa gharama ya Sh80 milioni.

Bustani hiyo ambayo ni ya pili ya kuvutia ufuoni mwa Bahari Hindi eneo la Pwani baada ya ile ya Mama Ngina jijini Mombasa, itakuwa na uwanja wa soka, mpira wa vikapu, mikahawa, maduka na viti vya kubarizi.

Pendekezo kuhusu marufuku ya nguo fupi, pombe na sigara lilikuwa limetolewa na kikundi cha kutetea haki za wakazi cha Okoa Malindi.

Viongozi wa kikundi hicho waliwasilisha mapendekezo yao kwa wasimamizi wa wadi ya Shela, Bi Zamzam Ali, manisipaa ya Malindi na Kaunti ya Kilifi.

Katibu Mkuu wa Okoa Malindi, Bw A.N Farhan alisema jamii ya Waswahili mjini Malindi haipo tayari kuruhusu bustani hiyo iwe na biashara yoyote ya vileo na sigara.

You can share this post!

Google yaipa Kenya Sh1.1 bilioni ijikwamue baada ya...

Presha kwa Raila akae kando 2022 aachie wengine