• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
Miradi ya barabara na maji safi kuwafaa wakazi wa Kiambu

Miradi ya barabara na maji safi kuwafaa wakazi wa Kiambu

Na LAWRENCE ONGARO

KAUNTI ya Kiambu imeweka mikakati ya kuchimba visima vya maji katika wadi kadha za eneo hilo.

Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro alisema serikali yake imetenga takribani Sh100 milioni ili kuchimba visima vitano katika eneo hilo.

Visima hivyo viko katika wadi za Juja, Theta, Nyachaba, Matangi, na Gachororo.

Aliwahakikishia wakazi hao kuwa bwawa la Kariminu lililoko Gatundu Kaskazini likikamilika, litatosheleza mahitaji ya kaunti nzima ya Kiambu na upatikanaji wa maji safi “itakuwa ndoto ambayo imetimia.”

“Ninawahakikishia kuwa ujenzi wa mradi wa maji wa bwawa la Kariminu utakapokamilika, wakazi wote wa Kiambu watanufaika pakubwa na maji hayo,” alisema Dkt Nyoro.

Aliwashauri wakazi wa Ruiru wasipotoshwe na siasa kwani kwa muda wa mwaka mmoja na nusu unaosalia kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 “nitahakikisha miradi yote inakamilika haraka iwezekanavyo.”

“Nyinyi kama wakazi wa hapa Ruiru msikubali kupotoshwa na siasa duni kwani lazima tuhakikishe Ajenda Nne Kuu za Rais Uhuru Kenyatta zinatimizwa,” akasema.

Aliyasema hayo mnamo Jumamosi alipozuru maeneo ya Juja na Ruiru ili kujionea miradi tofauti ya maendeleo.

Alizuru Juja ili kukagua ukarabati wa barabara ya JujaFarm ya umbali wa kilomita 12 huku wakitarajia kukamilisha kilomita tatu chini ya majuma mawili.

Alisema serikali kuu inafanya juhudi kuona ya kwamba barabara hiyo inakamilika haraka iwezekanavyo ili kupunguza msongamano wa magari unaoshuhudiwa kila mara.

Wakazi wa Juja na Ruiru kwa muda mrefu wamekuwa na shida ya maji na barabara huku wakipata shida televmsimu wa mvua.

Bi Margaret Wanjiru wa kijiji cha Theta anasema wamekuwa wakitafuta maji mwendo mrefu lakini kisima walichochimbiwa kitawanufaisha pakubwa.

“Sisi kama wakazi wa hapa tunashukuru serikali ya kaunti kwa kutujali kuona ya kwamba tunastahili kupata maji haraka iwezekanavyo,” alisema Bi Wanjiru.

James Kimani ambaye ni mkazi wa kijiji cha Matangi, Ruiru alisema shida ya maji katika eneo hilo itakuwa ni historia kwani wakazi wote watanufaika na kisima kilichochimbwa.

You can share this post!

Ronaldo awabeba Juventus dhidi ya Udinese katika Serie A

Mashabiki watibua mechi ya EPL kati ya Man-United na...