• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:47 PM
Mjukuu wa Moi adai hana uwezo kulea watoto

Mjukuu wa Moi adai hana uwezo kulea watoto

Na JOSEPH OPENDA

MJUKUU wa aliyekuwa Rais (mstaafu) Mzee Daniel Moi, anayekabiliwa na kesi inayohusu Sh1 milioni kila mwezi kugharamia malezi, sasa anasema hana uwezo wa kuwajibikia malezi ya watoto wake wawili.

Bw Collins Kibet Moi alieleza Korti ya Nakuru kuwa, hana namna ya kutimiza matakwa ya mkewe waliyetengana Gladys Jeruto Tagi, ya kugharimia Sh1 milioni kila mwezi kuhusu malezi ya watoto akisema hana kazi wala mapato yoyote.

Kupitia nakala rasmi ya majibu yake iliyowasilishwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Nakuru Benjamin Limo, Bw Kibet alisema anaweza tu kugharimia matibabu ya watoto kwa kuwalipia ada ya kila mwaka ya Bima ya Hospitali Nchini (NHIF).

Alipendekeza vilevile watoto hao wahamishwe katika shule ya umma, Shule ya Msingi ya JK, Eldama Ravine, Baringo, akisema ndiyo pekee anayoweza kumudu.

“Kwa sasa nimelemewa kifedha hivyo basi sina uwezo wa kutoa zaidi ya kile ninachotaja hapa na mlalamishi ambaye ni jirani yangu wa karibu nyumbani anafahamu hili vyema,” alisema Bw Kibet.

Amedai yeye ni mwanamume maskini asiye na namna ya kujipatia riziki na anayewategemea marafiki na jamaa kujikimu kimaisha.

Alielezea mahakama kwamba, amekuwa akiugua matatizo ya kiakili na aliachiliwa hivi majuzi kutoka kituo cha kurekebisha tabia alipokuwa akitibiwa kutokana na mazoea ya kubugia pombe.

Alikanusha kwamba aliwahi kumwoa Bi Jeruto akisema hakuwa na akili sawa wakati walipokuwa kwenye uhusiano uliosababisha kuzaliwa kwa watoto hao wawili.

Mwanamme huyo amedai kuwa na watoto wawili alioachiwa baada ya talaka na kukanusha kwamba aliwahi kuishi na Bi Jeruto Kenya na Uswisi.

“Kutokana na hali yangu ya kuugua kiakili ambayo imesababisha kupoteza biashara, fedha zangu binafsi zimeathiriwa pakubwa kiasi kwamba ninategemea marafiki na jamaa kukidhi mahitaji yangu,” alisema Bw Kibet.

Alikabiliwa na kesi mnamo Machi baada ya Bi Jeruto kwenda kortini akimshutumu dhidi ya kutelekeza wajibu wake kama mzazi.

You can share this post!

Muturi adai uhasama umeathiri Bunge

IPOA yaripoti ongezeko la idadi ya malamishi dhidi ya polisi