• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Mke wa Rais, mke wa DP wazindua mpango wa usambazaji chakula Mukuru

Mke wa Rais, mke wa DP wazindua mpango wa usambazaji chakula Mukuru

NA SAMMY KIMATU

MKEWE Rais William Ruto na mkewe naibu wa rais Bw Rigathi Gachagua, Bi Rachel Ruto na Pasta Dorcas Wanjiku Gachagua mtawalia, walianza mpango wa kusambaza chakula cha msaada mwishoni mwa wiki.

Katika hafla iliyofanyika katika uga wa Railway Training Institute (RTI), wawili hao walizindua mpango wa kugawa chakula cha msaada kutoka kwa serikali kuu.

Bi Ruto aliwaambia maelfu ya wakazi wa mitaa ya mabanda ya Mukuru ilioko tarafani South B, kaunti ndogo ya Starehe watagawiwa chakula na machifu wao.

Zaidi ya hayo, mkewe rais aliahidi kujenga hospitali kwa wakazi wa South B akisema kuna umuhimu wa wakazi kuwa na hospitali karibu na makazi yao badala ya kutafuta huduma ya matibabu kutoka mbali.

Aliongeza kwamba atazuru mitaa ya mabanda ya Mukuru na kutangamana na wakazi na kusikiza huduma wanazohitaji kufanyiwa na serikali.

Wakati huo huo, Bi Ruto aliagiza gavana wa Nairobi Bw Johnson Sakaja kujenga daraja la Kaiyaba/Hazina ambayo imekuwa kero kwa miaka mingi.

Hoja ya ukosefu wa daraja katika maeneo hayo ililetwa na mwakilishi wa wodi ya landi Mawe, Bw Simon Mugo Maina almaarufu Miche Miche.

Mkutano huo ulihudhuriwa na mbunge wa Starehe, Bw Amos Mwago na mwakilishi wa wadi ya Landi Mawe, Bw Simon Maina Mugo.

Awali, wakazi walikuwa wameagizwa na machifu kufika katika Shule ya Msingi ya Mukuru kupatiwa mgao wa chakula.

Baadaye, waliambiwa tena hafla ilibadilishwa na hivyo haitafanyika shuleni Mukuru bali itakuwa katika uga wa Taasisi ya Mafunzo ya Reli Nchini (RTI).

“Tulirauka mapema ili tukipanga foleni tume miongoni mwa watu 100 wa kwanza lakini tukavunjika moyo kuambiwa baadaye kwamba mahali pa kupatiwa chakula ni RTI wala sio Mukuru,” Bi Alice Khalumba akasema.

Hata hivyo, walipoenda RTI walikuta chakula kimejaa ndani ya malori lakini wakaahidiwa na mkewe wa rais kwamba baada ya uzinduzi wa chakula kukamilika, watapata chakula kupitia kwa machifu.

Akiongea jana Jumatatu na Taifa Leo, chifu wa Mukuru Nyayo, Bw Charles Mwatha alisema mpango wa kugawia wananchi chakula haukufanyika Shuleni Mukuru jwa sababu hakukuwa na nafasi ya kutosha watu wengi.

“Mahali pa kusambazia chakula kulibadilishwa dakika za mwisho mwisho kutoka Shuleni ya Msingi ya Mukuru na kupelekwa RTI kwa sababu RTI kuna uga wa kutoshea watu wengi,” Bw Mwatha akasema.

Hata hivyo, maelfu ya wakazi wakiwa na mifuko na gunia za kuwekea chakula walirudi nyumbani wakinung’unika na kukata tamaa.

You can share this post!

TAHARIRI: Magavana wasifiche maovu ya watangulizi wao

Mawaziri wa Ruto waropokwa ovyo

T L