• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
TAHARIRI: Magavana wasifiche maovu ya watangulizi wao

TAHARIRI: Magavana wasifiche maovu ya watangulizi wao

NA MHARIRI

MAGAVANA walioingia mamlakani baada ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti, wanafaa kutendea haki wananchi kwa kusaidia kulinda mali zote za umma.

Katika baadhi ya kaunti ambazo zilipata magavana wapya, viongozi hao waliingia kwa mbwembwe tele wakionyesha nia ya kuleta mabadiliko.

Mabadiliko makuu yalilengwa katika sekta ya fedha na ajira za wafanyakazi.

Kuna magavana waliounda kamati maalumu ili kuchunguza matumizi ya fedha katika serikali za watangulizi wao huku pia wakitaka kujua idadi halisi ya wafanyakazi. Hii ni kwa sababu kiasi kikubwa cha fedha za umma hutengewa mishahara, marupurupu na malipo mengine ya wafanyakazi serikalini.

Kufikia sasa, imeanza kufichuka katika baadhi ya kaunti hizo kwamba kuna uwezekano wa ufujaji wa mabilioni ya fedha uliotendeka hasa kupitia kwa ulipaji mishahara kwa wafanyakazi hewa.

Ijapokuwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) ilikuwa inachunguza awali magavana kadha walioondoka, magavana walioingia mamlakani wana jukumu muhimu kuhakikisha haki inatendeka hasa ikibainika fedha zilifujwa.

Hatungependa kuona hali ya kwamba magavana walio mamlakani watataka kutumia mamlaka yao kuwalinda wenzao walioondoka.

Tunajua kuna kaunti ambapo magavana walioingia ni wandani wa wale ambao waling’atuka.

Hii haifai kutumiwa kama kigezo cha kuficha ushahidi kuhusu wizi wa pesa ambazo zingesaidia kutatua changamoto nyingi zinazokumba raia.

Huwa inaudhi sana kuendelea kuona magavana, mawaziri wa kaunti, maafisa wakuu, madiwani na wafanyakazi wengine walio na ushawishi katika kaunti pamoja na wandani wao wakiishi maisha ya kifahari wakati ambapo wakazi wa kaunti hizo wanataabika.

Hakuna tatizo kama pesa zinazofadhili maisha hayo zilipatikana kwa njia za haki. Lakini kama ni maisha yanayogharamiwa na raia anayelala njaa na kukosa huduma muhimu anazohitaji, hilo si tofauti na laana kwa kiongozi husika.

Ni matumaini yetu kwamba kila kaunti iliyounda jopo la kuchunguza idara muhimu za watangulizi wao zitatoa ripoti zao wazi kwa umma.

Vilevile, tunatumai kwamba magavana waliopo watajitolea kusaidia asasi nyingine zozote ambazo zinaendeleza uchunguzi huru.

Changamoto nyingi za tangu jadi katika jamii zinaweza kutatuliwa haraka ikiwa tutakuwa na viongozi waliojitolea kutumia vyema rasilimali za umma.

Hii inafaa ianzie katika usimamizi bora wa fedha ambazo huwa zinapokewa katika kaunti kila mwaka.

Kufikia sasa kuna kaunti ambazo zimepokea mabilioni ya pesa tangu mwaka wa 2013 ilhali hakuna maendeleo yoyote ya kuridhisha yanayoonekana.

You can share this post!

Mradi wa nyumba wa Buxton kuingia awamu ya pili

Mke wa Rais, mke wa DP wazindua mpango wa usambazaji...

T L