• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 1:05 PM
Mkulima anavyochuma kwa mimea na ufugaji samaki

Mkulima anavyochuma kwa mimea na ufugaji samaki

Na PETER CHANGTOEK

ENEO la Kyuso-Ngomeni, katika Kaunti ya Kitui, ni eneo linalokumbwa na kiangazi mara kwa mara. Hata hivyo, kiangazi kinacholikumba eneo lilo hilo, hakijamzuia Josiah Safari kuyaendeleza masuala ya kilimo.

Ni mkulima hodari ambaye hushughulika na ukuzaji wa mimea mbalimbali kama vile mipapai, mitikiti, pilipili mboga miongoni mwa mimea mingineyo.Aidha, Safari hushughulikia ufugaji wa samaki. Anakitumia kidimbwi alichokitengeneza ambacho si kirefu kwa kina, kuwafuga samaki.

Kwa jumla, ana shamba ekari kumi, lakini hulitumia shamba ekari tatu kuziendesha shughuli za kilimo.Anasema kuwa, amekuwa na ndoto ya kuendeleza kilimo-biashara, ambacho ni chenye manufaa, katika maisha yake, na kuwatia moyo wakulima wanaoishi katika eneo hilo, ambalo hukabiliwa mno na ukame.

Hapo awali, alikuwa akifanya biashara ya hoteli. Hata hivyo, ukosefu wa maji ulimshurutisha kuchimba kisima cha kina kifupi.“Nilishangaa kupata maji mengi yaliyo safi kuliko nilivyokuwa nikitarajia. Nikaamua kuweka paipu na kusambaza maji katika kituo cha biashara kilichoko karibu,” aeleza Safari, akiongeza kuwa, aliyasambaza maji hayo, pia, nyumbani kwake na kuyasambaza pia kwa majirani.

Alipoona kuwa alikuwa na maji mengi, akaamua kuyatumia katika shughuli za kilimo. “Maji yalikuwa mengi, na hivyo ndivyo nilivyojitosa katika shughuli za ukulima. Nikaanza kuikuza mitikiti na pilipili mboga, kwa kutumia mbinu ya unyunyiziaji maji,” afichua mkulima huyo, ambaye alijitosa katika zaraa miaka mitano iliyopita.

PICHA:
Safari, akionyesha samaki waliovuliwa kwa kidimbwi chake.

Anasema kuwa, mazao hayo hayakuwa yakipatikana kwa urahisi katika eneo hilo, na yalikuwa yakihitajika mno, na alikuwa akiwauzia wateja waliokuwa wakitoka katika miji iliyoko karibu, kama vile Mwingi.

“Mimi hutumia rununu yangu kuwasiliana na kuwasiliana na wafanyakazi wangu watatu shambani,” asema, akiongeza kuwa, kwa wakati fulani, huwaajiri wahudumu 30 shambani wakati ambapo nguvukazi inahitajika kwa wingi.

Yeye hufanya utafiti mitandaoni, ili kuwa na habari na ufahamu mwingi kwa masuala ya kilimo. Mbali na kufanya utafiti mitandaoni, mkulima huyo huyauza mazao yake kupitia kwa majukwaa yayo hayo.

Mkulima huyo anawashauri wale wanaotaka kujitosa katika shughuli za zaraa kufanya utafiti kuhusu soko la mazao kwanza, kabla hawajajitosa katika shughuli zenyewe.Anaongeza kuwa, iwapo mkulima anaelewa fika kuhusu soko la mazao yake yanayohitajika, watanufaika.

“Kwa upande wangu, nimekuwa nikiikuza mimea ya pilipili mboga kwa muda wa miaka minne, lakini nimeongezea mimea mingine kama vile mipapai,” asema mkulima huyo.Safari huikuza mipapai inayojulikana kwa jina Malkia. Aina hiyo ya mipapai hukua upesi sana. Aina hiyo ya mipapai huchukua muda wa miezi tisa hadi kumi na miwili kukua na kuanza kuwa na matunda.

Aidha, mkulima huyo, huwafuga samaki ambapo ana kidimbi kilicho na samaki wengi. Anasema kuwa amewauza kadha wa kadha na kutia kibindoni kiasi kikubwa cha fedha.Kwa sasa, Safari, ambaye huwafuga samaki aina ya tilapia, ana samaki 2,500 waliomo kidimbwini, na humwuza samaki mmoja kwa Sh100-Sh250, kwa kutegemea ukubwa.

PICHA:
Samaki aina ya tilapia waliovuliwa na Safari.
  • Tags

You can share this post!

Hatari ya Sagana River Water Fall, Muruguru – Nyeri

Adhabu ya Onana aliyepigwa marufuku kwa miezi 12 yapunguzwa...