• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
Msako kuzima tabia ya uunganishaji stima kinyume cha sheria

Msako kuzima tabia ya uunganishaji stima kinyume cha sheria

Na SAMMY KIMATU

SERIKALI imeendeleza msako dhidi ya uunganishaji stima kinyume cha sheria katika mitaa yote ya mabanda iliyoko Kaunti ya Nairobi.

Hatua hii imelemaza biashara nyingi miongoni mwa wakazi wa mitaa lengwa hasa kwa wanaotumia stima kufanya kazi.

Aidha, walioathirika zaidi ni mafundi wa sekta ya juakali wanaotengeneza bidhaa kwa kutumia stima.

Wengine ni wamiliki wa saluni, vinyozi na vibanda vya kuuza vyakula huku wauzaji nyama katika bucha wakikadiriria hasara baada ya nyama kuharibika.

“Kwa kawaida, huwa nikihifadhi nyama ndani ya jokovu lakini baada ya kukosa stima, nyama imeharibika,” Muuzaji nyama mtaani wa mabanda wa Hazina akasema.

Baada ya transfoma kubebwa na wafanyakazi wa kampuni ya kusambaza stima nchini – Kenya Power – katika mtaa wa Mukuru-Sokoni, waliondoa transfoma nyingine mtaani Mukuru-Kayaba mwishoni mwa wiki.

Kando na msako wa kuondoa na kubeba trasfoma mitaani hiyo, walichukua zingine kutoka eneo la Sanasana kwenye maeneo ya Plainsview mtaani South B.

Isitoshe, katika mtaa wa mabanda wa Kayaba, walibeba trasfoma tatu kwa jumla.

“Transfoma moja ya mtaa wa Kayaba ilitolewa na kubebwa kutoka karibu na lango la shule ya Msingi ya Sancta Maria-Mukuru, nyingine karibu na steji ya Kayaba na transfoma ya tatu katika eneo la Lengo kwenye barabara ya Sigei,” Bw Jacob Ibrahim, mwenyekiti wa usalama mtaani Kayaba akaambia Taifa Leo.

Mapema mwaka 2020, wafanyakazi wa Kenya Power walichukua transfoma nyingine iliyokuwa ikihudumia wakazi katika mtaa wa Mukuru-Maasai na Mukuru-Hazina na kuwacha maelfu ya wakazi wakihangaika gizani.

Huku hayo yakijiri, waporaji nao wamefurahia hatua hiyo kwa kuchukua fursa ya kufanya uhalifu.

“Vijana wanavamia akinamama wanaorauka saa kumi kwenda sokoni kununua mboga. Washukiwa wa uhalifu huo hulenga kuiba pesa na simu kutoka kwa wamama wa biashara,” Bw Mulandi Mutua akasema.

Kwa wakati huu, mitaa ya mabanda ya Mukuru inayopatikana katika maeneo ya South B, Viwandani, Embakasi na kwingineko imo kwenye giza totoro.

Akiongea kuhusiana na matukio haya, mkuu wa tarafa katika eneo la South B, Bw Michael Aswani Were alisema nia ya serikali kufuatia misako hiyo ni kuwaletea wananchi stima safi na iliyo salama.

“Serikali ina nia ya kuwaunganishia wananchi stima ya kujilipia pesa wenyewe maarufu ‘tokens’ ambayo itakuwa ni safi na salama kwa matumizi yao ikilinganishwa na ile wakazi wanajiunganishia kinyume cha sheria,” taarifa ya Bw Were ikasema.

Kulingana na ripoti kutoka kampuni ya Kenya Power, kampuni hiyo imeripoti hasara ya mabilioni ya pesa kufuatia uunganishaji wa stima kiholela mitaani na ni kinyume cha sheria.

“Wakazi katika mitaa ya mabanda hulipishwa pesa nyingi na matapeli na mabroka huku pesa hizo zikiishia kwa mifuko ya watu wachache nayo Kenya Power ikipoteza hela,” Bw Were akadokeza.

Kutokana na ukosefu wa nguvu za umeme mitaani husika, wamiliki wa nyumba nao hawakusazwa kwani wapangaji wengi wameanza kuhama kwa mamia wakitafuta kukodi nyumba zilizounganishwa na stima mitaani mingineyo.

You can share this post!

Kenya U23 yakamilisha matayarisho ya Cecafa

Modern Coast kuingia vitani kuhakiklisha inabakia kwenye NSL