• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 11:48 AM
Mswada wazua hofu ya njama ya kuiba kura

Mswada wazua hofu ya njama ya kuiba kura

NA CHARLES WASONGA

KUNA wasiwasi kuwa mswada mpya unaobadilisha sheria kuhusu mfumo wa uwasilishaji matokeo ya uchaguzi wa urais ni njama ya kuiba kura katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Mswada huo wa marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi unalenga kuzuia Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) pamoja na vyombo vya habari kupeperusha matokeo moja kwa moja kutoka vituo vya kupigia kura kote nchini ilivyofanya katika chaguzi zilizopita.

Badala yake unapendekeza kuwa matokeo yote ya uchaguzi wa urais yawasilishwe katika kituo cha kitaifa cha kujumuisha kura jijini Nairobi, ili yatangazwe na mwenyekiti wa IEBC ndani ya siku saba baada ya kura kupigwa.

Hii ina maana endapo mswada huo utapitishwa bila kufanyiwa marekebisho yoyote, Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati ataruhusiwa tu kutangaza matokeo ya uchaguzi wa urais baada ya kupokea matokeo yote kutoka maeneobunge 290 nchini.

Vilevile, mswada huo, ambao umedhaminiwa na Kiongozi wa Wengi katika bunge la kitaifa Amos Kimunya unahalalisha uwasilishaji wa matokeo ya uchaguzi wa urais kwa njia ya nakala, mbali na ile ya kieletroniki.

“Maafisa wa kusimamia uchaguzi wanaweza kuwasilisha fomu za matokeo ya uchaguzi kwa kusafiri moja kwa moja hadi kituo cha kitaifa cha kujumuisha kura za urais na matokeo hayo yawe halali sawa na matokeo yaliyotumwa kielektroniki,” unasema mswada huo.

Hii ina maana kuwa maafisa wa kusimamia uchaguzi hasa wale walioko katika maeneo yasiyofikiwa na mawimbi ya mawasiliano ya 3G au 4G, watahitaji kusafiri hadi Nairobi kuwasilisha fomu za uchaguzi wa urais.

Mwanya wa wizi

Kulingana na sheria ya sasa na matokeo ya urais sharti yawasilishwe kwa njia ya kielektroniki pekee kutoka vituo vya kupigia kura hadi katika kituo cha kitaifa cha kujumuisha kura.

Kulingana na wachanganuzi wa siasa na watetezi wa utawala bora, mapendekezo hayo yanatoa mwanya wa wizi wa kura, na pia kuchochea ukosefu wa imani na matokeo, hali inayoweza kuzua taharuki na hata ghasia jinsi ilivyofanyika 2007.

Mkurugenzi wa kituo cha International Center for Policy and Conflict (ICPC), Ndung’u Wainaina aliwataja wanaopendekeza marekebisho hayo kama wachochezi wa ghasia walio na nia ya kutumia udhaifu huo kuvuruga uchaguzi mkuu ili kuhakisha wanayependelea ameshinda.

Kuhujumu katiba

“Wakenya wote wanaojali nchi hii sharti wasimame kidete kuwakataa wale wanaotaka kuhujumu Katiba na amani nchini,” akasema Bw Wainaina.

Wakili Miguna Miguna naye alisema utangazaji wa matokeo ya kura mara yanapochipuka ni njia bora ya kuhakikisha uwazi na uwajibikaji katika shughuli hiyo.

“Ni wezi pekee ambao wanaweza kuwa na nia ya kuwazuia Wakenya kufuatilia matokeo moja kwa moja. Lazima tupinge njama hizi,” akasema Bw Miguna.

Lakini wanaopendekeza marekebisho hayo wanajitetea kuwa mswada unalenga kuziba mwanya ambao Mahakama ya Juu ilitumia kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa urais wa 2017.

Wanasema kuwa mswada huo pia unatoa nafasi kwa IEBC kutambua wapigakura kwa kutumia sajili ya kawaida mbali na mtambo wa kielektroniki (BVR).

Kwa upande wao, wanasiasa wa mrengo wa Naibu Rais William Ruto wakiongozwa na Seneta wa Nandi Samson Cherargei na wabunge Nelson Koech (Belgut) na Caleb Kositany wamewataka wabunge kuangusha mswada huo, wakidai unalenga kufanikisha wizi wa kura kwa manufaa ya muungano wa Azimio la Umoja.

“Kwa kuwanyima wapigakura haki ya kufuatia matokeo ya urais kupitia runinga, mitandaoni na tovuti ya IEBC, sheria hii itasababisha taharuki na fujo. Kulingana na kipengele cha 35 cha Katiba, ni haki ya Wakenya kupata habari kutoka asasi za serikali bila kuwekewa vikwazo,” Bw Cherargei akasema Alhamisi asubuhi kwenye mahojiano katika runinga ya Citizen.

Kwa upande wao Mbw Koech na Kositany walisema wadhamini wa mswada huo wanaogozwa na malengo fiche ya kumsadia kiongozi wa ODM Raila Odinga kupata ushindi kwa njia ya udanganyifu.

“Hawa watu wameng’amua kuwa Raila hawezi kushinda uchaguzi kwa njia halali baada ya kutorokwa na waliokuwa wandani wake katika muungano wa NASA. Hii ndiyo maana sasa wanaleta sheria ya kuzuia vyombo vya habari kupeperusha matokeo moja kwa moja ili wapate mwanya wa kuiba kura. Tutapinga njama hii,” Bw Koech akaambia Taifa Leo kupitia ujumbe mfupi.

You can share this post!

CA yataka watangazaji wagombeaji kuacha kazi kufikia Aprili...

Serikali ya Kaunti yaahidi kuwasomesha watoto wa shabiki...

T L