• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:55 PM
Serikali ya Kaunti yaahidi kuwasomesha watoto wa shabiki Juma aliyeuawa

Serikali ya Kaunti yaahidi kuwasomesha watoto wa shabiki Juma aliyeuawa

NA JOHN ASHIHUNDU

SERIKALI ya Kaunti ya Kakamega imeahidi kugharimia maandalizi ya matanga ya shabiki nambari moja nchini Isaac Juma pamoja na kusomesha watoto wake watatu wa sekondari.

Fernandes Barasa anayewania kiti cha ugavana cha kaunti hiyo alikuwa ametoa ahadi kama hiyo ya kusomesha watoto wa marehemu aliyefariki baada ya kukatwakatwa na kuaga papo hapo nyumbani kwake wiki moja iliyopita.

“Juma alikuwa akinifanyia matangazo ya bure wakati wa mashindano yangu ya Barasa Foundation Championship katika maeneo yote 12 ya Kakamega. Alikuwa rafiki wa karibu ambaye nitampeza kwa kiasi kikubwa. Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi,” alisema Bw Barasa.

Gavana wa Kakamega, Wycliffe Oparanya alimkumbuka Juma kama shabiki sugu aliyependa timu ya taifa Harambee Stars pamoja na klabu ya AFC Leopards, huku akiitaka idara ya Polisi itie mbaroni wote waliohusika na kifo chake.

“Nimemfahamu Juma kwa miaka mingi tangu nikiwa afisa AFC Leopards. Alisafiri na timu safari kote nchini na hata katika mataifa ya kigeni kushangilia wachezaji na kutumbuiza mashabiki,” alisema Oparanya ambaye alikuwa katika afisi ya Ingwe kati ya 1992-1999 ambapo aliisaidia kutwaa mataji mawili ya ligi kuu miongoni mwa mengine mengi.

Alisema viongozi wa tabaka mbali mbali akiwemo kinara wa ODM Raila Odinga watahudhuria mazishi ya Juma mnamo Februari 12.

Shabiki sugu Jared Otieno Obonyo, maarufu kama Jaro Soldier ni miongoni mwa washika dau wakuu wanaotaka Serikali impe heshima zote marehemu Juma.

“Juma ameilifanyia taifa hili mengi makubwa kwa miaka mingi. Mbali na kuwa shabiki mkubwa wa soka, kadhalika alihudhuria mashindano ya riadha, na mechi za raga kushangilia timu mbali mbali. Ningependa Serikali kupitia kwa Wizara ya Michezo ihusike kikamilifu katika mazishi yake jinsi ilivyohusika Agnes Tirop wa rekodi ya Dunia katika mbio za kilomita 10 alipoaga,” aliongeza kiongozi huyo wa The Green Army.

  • Tags

You can share this post!

Mswada wazua hofu ya njama ya kuiba kura

JUMA NAMLOLA: Raila asipotoshwe; anaweza kushinda bila...

T L