• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
Mudavadi na Wetangula waombwa kuheshimu Malala

Mudavadi na Wetangula waombwa kuheshimu Malala

NA JESSE CHENGE

VIONGOZI wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) kutoka Bungoma wametoa wito kwa wenzao wa Ford Kenya na Amani National Congress (ANC) kuheshimu Katibu Mkuu wa UDA, Bw Cleophas Malala.

Wakiongozwa na mbunge wa Webuye Magharibi, Bw Dan Wanyama, wanalalamikia kudhalilishwa kwa Katibu Mkuu huyo wa chama tawala kinachoongozwa na Rais William Ruto.

“Tunawezaje kuwa na nguvu na umoja kama jamii ikiwa hatuheshimiani? Ni lazima tukubaliane kwamba Bw Cleophas Malala ndiye Katibu Mkuu wetu na anastahili heshima kutoka kwa kila mmoja wetu,” akasema mbunge huyo.

Bw Wanyama alitoa wito huo mnamo Jumapili, Septemba 24, 2023 katika hafla ya kuchangisha pesa za kanisa eneo la Mlima Elgon, iliyohudhuriwa na Malala na viongozi wengine kutoka Magharibi mwa Kenya.

Mbunge wa Mlima Elgon, Fred Kapondi naye alisema: “Tunapaswa kuacha tofauti zetu za kisiasa na kuzingatia maslahi ya watu wetu. Malala amekuwa akishirikiana nasi vyema katika kuwahudumia wapiga kura wetu. Ni wajibu wetu kuheshimu nafasi na ofisi yake na kumpa ushirikiano anaohitaji.”

Kulingana na viongozi hao, kuna ukosefu mkubwa wa heshima kwa Malala, hasa kutoka kwa wanachama wa ANC na Ford-Kenya, akisisitiza kwamba ni jambo lisilokubalika.

Aidha, wanasiasa hao wa Magharibi mwa Kenya walitishia kuondoa msaada wao kwa wanaoendelea kumdharau Katibu Mkuu huyo wa UDA.

Aidha, wametaka umoja na utangamano miongoni mwa viongozi wa Magharibi mwa Kenya na kuwasihi kufanya kazi kwa pamoja kwa lengo la kulinda maslahi ya watu katika eneo hilo.

Bw Wycliffe Wangamati, aliyekuwa Gavana wa Bungoma, alitoa onyo kali kwa wanaomdhalilisha Malala, akisema, “Kuna mipaka inayopaswa kuangaliwa na kuheshimiwa. Hatuwezi kuendelea kuwawakilisha watu wetu vizuri ikiwa hatutaheshimiana kama viongozi. Tunapaswa kutambua kuwa Bw Malala ni mmoja wetu na tumsaidie katika kutekeleza majukumu yake ya chama cha UDA.”

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Gavana Kawira roho mkononi UDA ikiunga mkono abanduliwe

Makahaba Nakuru walalamikia kutwangwa viboko na wazee wa...

T L