• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 3:55 PM
Mvua yazua mafuriko na yaletea wakazi hasara

Mvua yazua mafuriko na yaletea wakazi hasara

NA WAANDISHI WETU

MAFURIKO makubwa yaliendelea kushuhudiwa katika sehemu mbalimbali nchini, hali ambayo imesababisha uharibifu wa miundomsingi na kuwaacha Wakenya wengi bila makao.

Jijini Nairobi, wakazi jana waliamkia misongamano ya magari baada ya mvua kubwa kunyesha usiku kucha hapo Jumapili.Baadhi ya magari yalianguka kwenye mitaro ya barabara zinazoendelea kujengwa, huku baadhi ya wakazi wakilalamika kupitia barabara zilizojaa maji wakielekea kazini mwao.

Katika kaunti ya Baringo, mamia ya familia katika vijiji vya Sintaan, Majindenge na Loboio eneo la Baringo Kusini waliachwa bila makao, baada ya nyumba zao kusombwa na mafuriko kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha eneo hilo.

Mafuriko hayo yalitokea baada ya mito Perkerra na Loboi kuvunja kingo zake na kuyafanya maji kuelekea katika makazi yaliyo karibu.

Bi Mary Lenaseku, ambaye ni mkazi kutoka eneo la Sintaan, alisema kuwa baadhi ya wakazi bado wanakadiria hatua watakazochukua baada ya kuathirika.

Wengine wamelazimika kutafuta hifadhi katika maeneo ya juu kama Marigat.Katika Kaunti ya Homa Bay, familia 170 zimeachwa bila makao kwa siku tatu zilizopita kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha.Kamishna wa kaunti hiyo, Bw Moses Lilan, alisema wamewashauri watu walioathiriwa kwenda katika maeneo ya juu.

Wanderi Kamau, Florah Koech na George Odiwuor

You can share this post!

Hakimu atoa uamuzi wake kwa Kiswahili sanifu

Kenya yasitisha safari za ndege Somalia