• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 8:50 AM
Mwanamke ashtakiwa katika kisa ambapo mpenziwe alifariki wakifanya mapenzi

Mwanamke ashtakiwa katika kisa ambapo mpenziwe alifariki wakifanya mapenzi

Na JOSEPH NDUNDA

Mwanamke wa umri wa miaka 28 ameshtakiwa kwa kumuua mpenzi wake ambaye aliaga dunia katika hali ya kutatanisha wakati walipokuwa wanafanya mapenzi ndani ya nyumba yake.

Winfred Mueni ameshtakiwa kwa mauaji ya kutokusudia kinyume na kifungu 202 kikisomwa pamoja na kifungu 205 cha Makosa ya Jinai ambapo anashukiwa kumuua Titus Njoroge Kimani, 30, katika mtaa wa Baba Dogo, Ruaraka, mnamo Septemba 22, 2023.

Mueni anashtakiwa kwa kukatiza maisha ya Kimani ambaye alipoteza fahamu na kuanguka akafa alipokuwa anafika kileleni wakati wa tendo la huba, ingawa alijaribu kumkimbiza hospitalini ambapo aliambiwa alishaaga dunia tayari.

Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma inamshtaki Mueni kama “mtu wa mwisho kuonekana na marehemu” kabla ya kifo chake.

Sheria hiyo inatoka Mahakama Kuu ya Nigeria inayotokana na kesi ya Stephen Haruna na Mkuu wa Sheria (2012).

Uamuzi huo unatokana na Mahakama Kuu ya Abuja iliyomfunga mshukiwa Oktoba 6, 2008 kwa kosa la kusababisha maafa.

Kwenye kesi hiyo, Haruna ambaye alikuwa bawabu katika makazi ya marehemu alipatikana na hatia ya mauaji yake kwa msingi wa kuwa ni yeye pekee aliyekuwa kwenye makazi hayo wakati wa kifo cha mwenye nyumba.

Mahakama ilibaini kwamba hakukuwa na ushahidi wa kuvunjwa kwa lango la mwendazake, na kwamba Haruna alikuwa mtu pekee kwenye makazi hayo.

DPP anaamini kwamba Mueni anastahili kushtakiwa kwa msingi huo akisema kesi yake inafanana na ya Haruna, licha ya kuwa hakuna ushahidi wowote kuonyesha kwamba alimsababishia majeraha wakati walipokuwa wanafanya mapenzi.

Upande wa mashtaka umeorodhesha mpira wa kondomu uliotumika ambao ulipatikana kando ya kitanda na ripoti ya upasuaji kama ushahidi mkuu dhidi ya Mueni na mumewe ameorodheshwa kama shahidi dhidi yake.

Kisa hiki ambacho kimekuwa kikichunguzwa kwa zaidi ya mwezi mzima kimeleta mgongano baina ya maafisa wa upelelezi (DCI) na wale wa mashtaka (ODPP).

Baada ya uchunguzi wa kina, DCI walikuwa wamependekeza vikao vya wazi vya kubaini alivyofariki Kimani kwa sababu hakukuwa na ushahidi wa kumhusisha yeyote moja kwa moja na kifo hicho.

Kwa mfano, mwili wa Kimani haukuwa na majeraha yoyote wakati ambapo marafiki na jamaa walimpata kitandani punde baada ya Mueni kuwaita mara moja baada ya mchezo mzito wa huba saa mbili asubuhi.

Maafisa wa upelelezi wa DCI ambao walielekea katika nyumba ya Kimani mara moja baada ya kujulishwa na hospitali kwamba ameshafariki walipata kila kitu kikiwa mahali pake.

Nyumba yake ilikuwa na kitanda, viti na mahali pa jikoni na hakukuwa na dalili zozote za mvurugano.

Lakini ODPP ilikosoa DCI kwa kutochukua chembechembe za mwili wa mwendazake zikakaguliwe kubaini haswa kilichomuua na ndipo akapendekeza Mueni ashtakiwa kwa mauaji ya kutokusudia.

Maafisa wa upelelezi wanaofahamu kuhusu kisa hiki na ambao hawakutaka kutajwa majina kwa sababu hawana ruhusa ya kuongea na vyombo vya habari wanasema kwamba hakukuwa na haja ya kuchukua chembechembe kwa sababu ripoti ya upasuaji tayari ilikuwa ishabaini chanzo cha kifo cha Kimani.

Dkt Peter Ndegwa, mwanapatholojia aliyefanya upasuaji huo katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya KUTRRH alibaini kwamba Kimani alifariki kutokana na jeraha la kichwa lililosababishwa na kifaa butu.

Mueni na Kimani walikuwa wameachana usiku uliotangulia. Alikuwa ameenda kwa kilabu cha pombe kumtafuta mumewe na akampata akiwa na watu wengine wakipanga mazishi. Mkutano huo uliisha saa saba usiku na mumewe Mueni aliondoka kwenda nyumbani akamwacha Mueni akinywa na marafiki. Hapo ndipo mpenziwe Mueni alifika na wakaendelea kunywa pombe pamoja.

Baadaye saa tisa asubuhi, wote waliondoka, Mueni akaenda nyumbani akampata mumewe akilala, wakalala.

Wakaamka baadaye saa kumi na mbili asubuhi wakala kiamsha kinywa na mumewe akaondoka kwenda kwa mazishi, Limuru, Kaunti ya Kiambu.

Hapo napo Mueni akaondoka nyumbani saa moja asubuhi kwenda kwa mpenziwe kushiriki mchezo wa huba.

Mshukiwa huyo ambaye anafanya kazi ya saluni amekuwemo kwenye ndoa kwa miaka miwili lakini amekuwa na mapenzi ya pembeni na Kimani.

Nje ya nyumba, alikutana na kaka mkubwa wa Kimani na mjomba wake ambao aliwasalimia na kuzungumza kwa kifupi kabla ya kuingia ndani ya nyumba ya mwendazake.

Kimani aliondoka kwenda kununua pakiti ya kondomu na akarejea kisha wakaanza kurushana roho.

Lakini kwa bahati mbaya, kulingana na simulizi ya Mueni kwa DCI, Kimani alipokuwa anafika kileleni, alianza kupatwa na matatizo ya kupumua, akaanza kukohoa na kuishiwa na nguvu akiwa amemlalia.

Aliambia wapelelezi kwamba aliendelea kuishiwa na nguvu hata zaidi na akazimia na kugonga kichwa kwenye fremu ya kitanda na kupoteza fahamu.

Mueni alichomoka kwenye nyumba akipiga mayowe na kuita jamaa wa Kimani ambao walimpata akiwa hana fahamu na akiwa uchi.

Alikimbizwa hospitalini ambapo alipatikana kwamba ashafariki na jamaa wakamsindikiza Mueni katika kituo cha polisi cha Ruaraka ambapo alitiwa mbaroni.

Alifikishwa katika Mahakama ya Makadara Novemba 10 ambapo alikanusha mashtaka mbele ya Hakimu Mkuu Hellen Okwani. Akaachiliwa kwa dhamana ya Sh500,000 na mdhamini wa kiasi sawa.

Kesi itatajwa Februri 22 na kuanza kusikizwa Mei 30, 2024.

Jamaa wa Kimani ambao walimuona Mueni akiingia nyumba ya Kimani na wafanyakazi wenzake ambao walifika nyumbani alipopiga mayowe wameorodheshwa kuwa mashahidi.

  • Tags

You can share this post!

Maji ya mafuriko yatatiza usafiri katika barabara kuu ya...

Wahudumu wa maboti waomba serikali iruhusu mtu kuchukua...

T L