• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Mwanamke ashtakiwa kuishi na jambazi na kukosa kuarifu polisi

Mwanamke ashtakiwa kuishi na jambazi na kukosa kuarifu polisi

NA JOSEPH NDUNDA

MWANAMKE mmoja mchanga amejipata mashakani baada ya kufunguliwa mashtaka kama mshiriki wa ujambazi kwa kukosa kufahamisha polisi kuwa mpenziwe alikuwa jambazi sugu aliyejihami.

Yvonne Muthoni, 19, alikamatwa katika nyumba ya mpenziwe Duncan Ndinya ambapo afisa wa polisi alipigwa risasi na kujeruhiwa katika ufyatulianaji risasi kabla ya kuaga dunia baadaye hospitalini.

Anatuhumiwa kupokea pesa na kadi za simu za kampuni mbalimbali za mawasiliano kutoka kwa Ndinya na washiriki wake baada ya kukubali kuficha tukio la wizi wa kimabavu lililotekelezwa na mpenziwe ambaye sasa ni marehemu.

Kwa sasa mshukiwa anachukuliwa kama mshiriki wa karibu wa Ndinya aliyeuawa kwa kupigwa risasi na makachero kutoka Idara ya Uchunguzi kuhusu Uhalifu (DCI) wakati wa ufyatulianaji ndani ya nyumba yake ya kukodisha eneo la Kasarani, Nairobi, mnamo Oktoba 8.

Alishtakiwa kwa kuzidisha matukio ya uhalifu kinyume na Kifungu 118 kikisomwa pamoja na Kipengee 36 cha Katiba na anatuhumiwa kutekeleza hatua hiyo mnamo Oktoba 8.

Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) vilevile imemshtaki Muthoni kwa kushirikiana na mtu anayemiliki bunduki kinyume na Kifungu 89 (2) cha Katiba.

Mshukiwa ameshtakiwa kwa kuishi pamoja na Ndinya aliyemiliki bastola aina ya Cesca nambari F9665 bila sababu thabiti, aliyotumia kumuua Konstebo wa Polisi Andrew Nyakundi.

Ndinya pia aliwapiga risasi na kuwajeruhi vibaya maafisa wenza watatu kutoka kitengo maalum cha DCI (OSU) ikiwemo Sajini Francis Singila, Makonstebo wa Polisi Joseph Karanja na Austin Nzioki Mutie.

Konstebo Nyakundi alifariki dunia kutokana na majeraha alipokuwa akipokea matibabu katika Hopsitali ya Nairobi West ambapo wenzake watatu wangali wamelazwa.

Maafisa hao walikuwa wanamfuata Ndinya aliyekuwa akisakwa kuhusiana na misururu ya visa vya ujambazi kote nchini, baadhi vilivyoripotiwa katika kaunti za Nairobi, Kajiado na Embu.

Maafisa wa DCI katika Kitengo cha Ujasusi kuhusu Uhalifu (CRIB) waligundua maficho yake Kasarani kabla ya kuvamia nyumba yake.

Muthoni alikanusha mashtaka mbele ya Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Makadara, Irene Gichobi na kuomba kuachiliwa kwa dhamana ya kiasi cha chini kupitia wakii wake Veinna Mongare aliyekubali kumwakilisha bila malipo.

  • Tags

You can share this post!

Manamba wa matatu mashakani kwa kumuibia na kumbaka mwanamke

Mkuu wa polisi Makadara athibitisha maafisa wa DCI...

T L