• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 2:24 PM
Mwanasosholojia aliyeanzisha kampuni inayoongeza thamani kwa viungo

Mwanasosholojia aliyeanzisha kampuni inayoongeza thamani kwa viungo

Na PETER CHANGTOEK

Uongezaji wa thamani kwa mazao ni biashara ambayo husaidia wakulima na wafanyibiashara kuongeza mapato wanayoyapata kutokana na bidhaa.

Aidha, mazao yaliyopitishwa kwa mchakato huo wa kuongeza thamani, huchukua muda mrefu pasi na kuharibika.Stephanie Njeri, 25, ni mmojawapo wa wafanyibiashara walioona mwanya katika mchakato huo, na akaamua kuanzisha kampuni ambayo huongeza thamani kwa bidhaa nchini, na kuwauzia wafanyibiashara wengine.

Kampuni yake inajulikana kwa jina Ukoo Farm Products, na huyanunua mazao yaliyozalishwa pasi na kuzitumia kemikali zozote, maathalan; pilipili, tangawizi, iliki, mdalasini, karafuu, n.k, na kuongezea thamani kwa kuyasaga mazao yenyewe, na kupakia kwa sacheti na mikebe na kuwauzia wateja mbalimbali.

Aliamua kujitosa katika shughuli ya kuongeza thamani kwa mazao ya viungo, kwa sababu wakulima wadogowadogo huwa hawana ujuzi wa kuongeza thamani kwa viungo hivyo.Stephanie huyanunua mazao hayo kutoka kwa wakulima walioko katika maeneo ya Nakuru, Nyeri, Meru, Mombasa, miongoni mwa maeneo mengineyo.

Anafichua kuwa, ili kuwafaidi wakulima wadogowadogo, huwanunulia mazao yao kwa bei zilizo juu kwa asilimia kumi, ikilinganishwa na bei zilizoko sokoni.“Sisi hununua tangawizi kilo 50 kwa kati ya Sh6,000 na Sh6,500, ikitegemea misimu. Hununua soya kwa Sh700-Sh900, pilipili manga kwa Sh8,000-Sh8,500, iliki kwa Sh6,700, karafuu kwa Sh6,200, mdalasini kwa Sh5,800 na jira kwa Sh6,400,” afichua, Stephanie, ambaye aliutumia mtaji wa Sh50,000 kuanzisha shughuli hiyo.

PETER CHANGTOEK
Bidhaa zilizoongezwa thamani, zitengenezwazo na Stephanie.

 

Kwa wakati huu, yeye hupeleka mazao hayo kusagwa katika kampuni nyingine. “Hata hivyo, tuna mashine ya kutengeneza mafuta ya nazi, na tutaanza kutengeneza mafuta hayo mwishoni mwa mwezi huu,” aongeza.

Anasema kuwa, mazao wanayoyanunua huzalishwa na wakulima hao pasi na kutumia kemikali. Aidha, anaongeza kuwa wakulima hao hutumia mbolea asilia na viuadudu asilia.Isitoshe, anadokeza kuwa, usafi hudumishwa na wakulima shambani, na huyanunua mazao yaliyo bora kutoka kwao.

Yeye huuza soya gramu 80 kwa Sh120, gramu 200 kwa Sh300. Pia, huuza gramu 80 za tangawizi kwa Sh150, na gramu 200 kwa Sh350. Vilevile, wao huuza pilipili manga zilizosagwa gramu 80 kwa Sh180 na gramu 200 kwa Sh400. Aidha, huuza gramu 80 za pilau masala kwa Sh180 na gramu 200 kwa Sh370.

Kwa wakati huu, ana wafanyikazi watatu na hutangaza biashara yake kupitia kwa mitandao ya kijamii k.v. Twitter na Instagram. Aidha, huziuza bidhaa zao kupitia kwa Jiji, Mkulima Young, Pigiame and Jumia.Kwa sasa, wao huziuza bidhaa zao katika Kaunti ya Nairobi tu, lakini iwapo wateja watamudu gharamu ya kusafirishiwa bidhaa hizo katika maeneo mengine ya nchi, wako tayari kuwauzia.

Kuna changamoto kadha wa kadha ambazo amewahi kuzipitia katika biashara hiyo, kama vile ukosefu wa fedha za kutosha za kuimarisha shughuli hiyo.Ananwasihi wale ambao wana nia ya kujitosa katika biashara kama hiyo, kuhakikisha kwamba wanatengeneza bidhaa zilizo bora, ili wawe na wateja kwa wingi.

Katika siku za usoni, anapania kuziuza bidhaa zake nje ya nchi. “Kenya ina uwezo mkubwa wa kuongeza thamani kwa mazao, hasa kwa sababu ni nchi inayotegemea kilimo,” asema Stephanie, akiongeza kuwa, anapanga kuanza kutengeneza mafuta ya nazi na yale ya maparachichi.

 

 

  • Tags

You can share this post!

Ukuzaji wa migomba aina ya TCB na Migimbi ulivyo na faida...

Kaunti zahimizwa kutengea sekta ya kilimo mgao wa fedha wa...