• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Mwenye kilabu cha Balle Balle taabani kwa kulangua wasichana tisa wa Nepal

Mwenye kilabu cha Balle Balle taabani kwa kulangua wasichana tisa wa Nepal

Na RICHARD MUNGUTI

MWENYE KILABU ambapo wasichana tisa kutoka nchi ya Nepal waliokolewa na maafisa wa polisi amejipata matatani kwa shtaka la ulanguzi wa binadamu.

Hakimu mkuu Francis Andayi alisema mkurugenzi wa mashtaka ya umma amewasilishas ushahidi dhidi ya Bw Sheikh Furoan Hussein kwamba alikaidi sheria za ulanguzi wa binadamu kwa nia ya kunyanyasa.

“Kulingana na ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka hii mahakama imefikia uamuzi kuna ushahidi wa kuwezesha korti kumtaka Hussain ajitetee,” Bw Andayi alisema.

Mahakama ilisema kiongozi wa mashtaka Bi Angela Fuchaka aliwasilisha ushahidi unaothibitisha haki za wasichana hao zilikandamizwa na Hussain.

Na wakati huo huo hakimu alimwachilia Bw Abduk Waheed Khan aliyeshtakiwa pamoja na Bw Hussain. Bw Andayi alisema ushahidi uliowasilishwa dhidi ya Bw Khan hauelezi jinsi alivyoshiriki katika kesi hiyo.

Bw Hussain alidaiwa ndiye mmiliki wa kilabu hicho lakini Bw Khan ndiye alikuwa anasimamia kilabu hicho cha Balle Balle.

Akitoa ushahidi Koplo Judith Kimungui alieleza korti polisi walipashwa habari kwamba wasichana wa umri mdogo walikuwa wananyanyaswa katika kilabu hicho cha Balle Balle kilichoko mtaani Parklands, Nairobi.

Koplo Kimungui alisema polisi walipofika mle kilabuni waliwapata wasichana hao wakinengua mauno huku wateja wengi wao wanaume wa asili ya kiheshia wakiwakondolea macho.

Kulikuwa na mikebe kumi ambayo ilikuwa inawekwa zawadi kwa mnenguaji hodari. Polisi walipoingia wasichana hao walitoroka na kujifungia ndani ya chumba kimoja kwenye kilabu hicho.

Pasipoti zao zilikuwa zimefichwa na Bw Hussain katika afisi yake. Mshyakiwa huyo ataanza kujitetea mnamo Feburuari 2 mwaka ujao.

You can share this post!

Watoto mayatima wafadhiliwa kuejerea darasani

Kibarua kigumu kwa wanavoliboli wa Kenya kimataifa