• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 12:52 PM
Mwenye mazoea ya kuibia wenye maduka ya Mpesa achapwa kama nguruwe

Mwenye mazoea ya kuibia wenye maduka ya Mpesa achapwa kama nguruwe

Na RICHARD MUNGUTI

MSHUKIWA wa wizi aliyetoroka mahakama ya Kibera Julai mwaka uliopita jana alipata kichapo cha nguruwe aliporudi kuiba kutoka duka la Mpesa katika eneo la Bus Station Nairobi.

Bw Isaiah Mugambi aliokolewa na Polisi kutoka kituo cha Kamukunji kabla ya kuuawa na wananchi waliokuwa na hasira kali. Mshukiwa huyo alipigwa na vifaa butu na marungu lakini akaokolewa na polisi.

Huku akivuja damu kichwani, mikononi na mdomoni, Bw Mugambi alitolewa shati na kuachwa na Vesti. Polisi walifika kabla ya kutiwa taya na kumwagiwa petrol awashwe moto.

Bw Mugambi alikuwa amemwibia mwanamke mwenye duka la Mpesa Sh30,000. Akiwa amejihami na kisu , Bw Mugambi alimvizia mwenye duka hilo lilio karibu na Benki ya Equity tawi la Knut House na kunyakua pesa hizo alipokuwa anazihesabu.

Mwanamke huyo alipiga kamsa. Wananchi walimkamata na kumchapa kwa kila aina ya vifaa. Alitandikwa barabara. Pesa alizokuwa ameiba zilipatikana. “Huyu mwanaume yuko na mazoea ya kuibia wenye maduka ya Mpesa katika eneo hili la Bus Station,” afisa wa polisi kutoka kituo cha Kamkunji aliambia Taifa Jumapili.

Afisa huyo alifichua kwamba kuna hati ya kumtia nguvuni Bw Mugambi iliyotolewa  na mahakama ya Kibera mnamo Julai 12, 2020 alipokosa kufika kortini wakati wa kusikizwa kwa kesi ya wizi wa Sh90,000 na simu yenye thamani ya Sh8,500.

“Ni kweli mshukiwa huyu aliniibia Feburuari 1,2020 na kutoroka,” Bi Christine Kyengo aliambia Taifa Jumapili. Polisi walisema mshtakiwa alitiwa nguvuni katika eneo la Kikuyu kaunti ya Kiambu baada ya kujificha kwa mwezi mmoja alipomwibia Bi Kyengo.

Alishtakiwa katika mahakama ya Kibera ambapo aliachiliwa kwa dhamana. Kesi hiyo iliorodheshwa kusikizwa Julai 12, 2020 lakini mshtakiwa hakufika kortini. Mbali na Bi Kyengo , mshtakiwa alitambuliwa na wenye maduka wengine kuwa mwenye mazoea ya kuiba katika eneo hilo la Bus Station.

“Kila anapoiba anaachiliwa. Huenda yuko na polisi wanaomlinda katika kituo cha Polisi cha Kamkunji,” mwenye duka mmoja alisema. Mnamo Feburuari 1 2020 ,Bw Mugambi alimwibia Bi Kyengo Sh90,000 na simu ya thamani ya Sh8,500.

Bw Mugambi alipelekwa na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Kamukunji akisubiri kupelekwa kortini wiki ijayo kufunguliwa mashtaka mapya. Mahakama itafutilia mbali dhamana aliyokuwa  ameachiliwa kisha azuiliwe katika gereza la viwandani hadi kesi mbili dhidi yake zisikizwe na kuamuliwa.

 

 

  • Tags

You can share this post!

Maafisa watatu wakuu wa polisi kujua hatma yao octoba 28

Washirika wa Ruto wapuuza chama kipya cha Lonyangapuo