• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Mwezi mzima bila masomo katika JSS

Mwezi mzima bila masomo katika JSS

NA WAANDISHI WETU

MWEZI mmoja tangu wanafunzi wajiunge na Sekondari ya Msingi (JSS), wengi wao katika shule za umma wamekuwa wakihudhuria leseni zao darasani, bila masomo kuendelea.

Umekuwa mwezi mzima wa kukaa bure, huku walimu wakuu na maafisa wa elimu wakijaribu kila mbinu kupata walimu wa kusaidia kufunza.

Shule nyingi maeneo mbalimbali nchini zinakumbwa na uhaba wa walimu, vitabu na miundomsingi duni.

Katibu wa chama cha Walimu (KNUT) tawi la Kakamega, Bw Tom Ingolo, anasema isipokuwa katika shule chache, kwa jumla wanafunzi wamepoteza mwezi mzima bila shughuli za masomo.

“Baadhi ya shule zina walimu wawili wa kufunza watoto 500. Walimu hao wawili watawezaje kufunza idadi hiyo kubwa?” akauliza.

Bw Ingolo aliambia Taifa Leo kwamba, ingawa masomo ya lazima ni 12, serikali imesambaza vitabu vya masomo matatu pekee – Home Science, Agriculture na Life Skills.

Katika kaunti ya Vihiga, Mkuu wa Elimu Bi Hellen Nyang’au alisema, walimu wa shule za msingi walio na diploma au digrii waliombwa kusaidia kufunza JSS.

“Walimu wakuu walizungumza na wale walio na diploma na digiri ili wasaidie. Kuna masomo 12 ambayo wanafunzi wanasoma,” akasema.

Hali si tofauti katika Kaunti ya Kisii ambako ingawa baadhi ya shule zimeanza masomo, walimu ni wachache.

Katika shule iliyoko Mogonga, eneobunge la Bomachoge Borabu, Tume ya Kuajiri Walimu (TSC), ilituma walimu wawili wiki mbili zilizopita.

Katika mojawapo ya masomo ambayo Taifa Leo ilihudhuria, mwalimu mpya alimaliza somo moja na hapo hapo akaanza kufundisha somo jingine.

“Inachosha. Sijabobea katika masomo yote lakini mumeniona nikichukua somo jingine. Hiyo ndiyo hali halisi. Tuko wawili tu hapa tulioletwa kwa ajili ya JSS lakini ni vigumu kusimamia madarasa matatu ambayo wanafunzi wanatakiwa kuchukua masomo 14,” alilalama mwalimu huyo mpya ambaye hakutaka kutajwa kwa kuhofia kuadhibiwa ilihali alipata kazi hivi majuzi.

Katika kaunti za Pwani, wakuu wa elimu walikiri kuna changamoto ya masomo katika Gredi 7 kwa sababu ya uhaba wa walimu na vitabu.

Mkurugenzi wa Elimu eneo la Pwani, Bw Luke Chebet alisema, kuna shule ambazo bado hazina walimu wa JSS, huku wanafunzi wakikosa vitabu vya kutosha.

“Tunaelewa kuwa kila kinachoanza lazima kiwe na changamoto. Mfumo huu wa CBC una changamoto zake lakini tunahakikisha tunazitatua hadi mwisho. Tunatatua hili kwa wiki mbili zijazo,” akasema Bw Chebet.

Alisema serikali imeanza kuajiri walimu zaidi katika shule hizo, na kuwasajili wanafunzi kwenye mfumo wa kidijitali ili kuwawezesha kupokea msaada wa fedha na vitabu kutoka kwa serikali.

Mkurugenzi wa Elimu Kaunti ya Lamu, Bw Joshua Kaaga, aliambia Taifa Leo kuwa, kati ya vitabu 12 vya Sekondari Msingi vinavyohitajika, kufikia sasa wamepokea viwili pekee.

Masomo pia hayajashika kasi Makueni, ambako baadhi ya walimu wakuu wamelazimika kutumia mbinu za kuvutia wanafunzi.

Katika shule ya msingi ya Itaava, eneobunge la Kibwezi Magharibi, wasimamizi wanaruhusu wanafunzi kuvaa sare walizotumia wakiwa Gredi ya 6. Mwenyekiti wa Bodi ya shule, Bw Benson Kamuti, alisema wamepata ufadhili wa madawati kutoka kwa Safaricom Foundation.

“Kilichosalia sasa ni kuanza kuchapa kazi ya kusomesha,” akasema.

Ripoti za Benson Amadala, Derick Luvega, Wycliffe Nyaberi, Siago Cece, Pius Maundu na Kalume Kazungu

  • Tags

You can share this post!

ZARAA: Kifaa cha mkono kuchuma chai, kupunguza gharama

EACC sasa yafuata utajiri wa Matiang’i

T L