• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:07 PM
ZARAA: Kifaa cha mkono kuchuma chai, kupunguza gharama

ZARAA: Kifaa cha mkono kuchuma chai, kupunguza gharama

NA SAMMY WAWERU

MOJAWAPO ya changamoto kuu inayogubika wakulima wa majanichai eneo la Githunguri, Kaunti ya Kiambu ni gharama ya uzalishaji.

Idadi ya wafanyakazi, hasa wachumaji ni ya chini wanaopatikana wakitolewa nje ya kaunti.

Samuel Njuguna, ni mkulima wa chai katika kata ndogo ya Mathanja, Githunguri mwenye uzoefu wa miaka 20 kukuza zao hilo.

Anasema endapo kuna mimea inayotajwa kuwa na mapato bora ingawa mambo nyanjani ni tofauti, ni majanichai.

Kilo moja kiwandani, kulingana na mkulima huyu inanunuliwa Sh21 eneo la Githunguri. Mapato hayo, mkulima anagawana na mfanyakazi – anayechuma.

“Kwa kila kilo, wachumaji wanalipwa Sh10. Hii ina maana kuwa, wafanyakazi wanapokea nusu ya mapato ya mkulima,” asema.

Usisahau gharama ya fatalaiza na kupalilia chai, yote ni ya mkulima.

Ni kwa sababu hiyo, Shirika la Ustawishaji Chai Nchini KTDA linaendelea kuhamasisha ukumbatiaji wa mifumo na teknolojia za kisasa.

Mojawapo, ni mashine ya mkono kuvuna chai.

Wenyeji Githunguri, eneo ambalo ni miongoni mwa yanayochangia kapu la chai nchini, wamefikiwa na mtambo huo wa kisasa.

Umeboreshwa, ambapo umeunganishwa na betri inayowekelewa mgongoni ikiwa kwenye mfuko.

Mmoja wa afisa wa KTDA kiwanda cha Kambaa, Githunguri aliyeomba kubana majina yake kwa sababu haruhusiwi kuzungumza na vyombo vya habari bila idhini, anasema mashine hiyo inahitaji watu wawili pekee.

“Mmoja ni wa kuvuna, na mwingine kuchagua chai ambayo imeafikia ubora,” aelezea.

Kwa siku, inavuna hadi kilo 150. Betri inahudumu kwa muda wa saa nane hadi kumi.

“Nikilinganisha utendakazi wake na wachumaji, inaonekana kurahisisha kazi. Kwa siku, mfanyakazi anayevuna kilo nyingi hazipiti 40,” Njuguna adokeza.

Mkulima huyu hulima chai kwenye ekari tano, na anasema wakati wa mavuno huandika vibarua watano.

Naye Nancy Njeri, anasema licha ya manufaa ya mashine hiyo, KTDA ina jukumu kuhakikisha wakulima wanapata mafunzo bora kuelewa kuitumia.

“Inavuna kila jani inalokutana nalo, hivyo basi kazi husalia kuchambua yale bora na yasiyotakikana,” asema mama huyo anayekuza chai katika ekari nne.

“Upotevu wa mazao, hususan kwa sababu ya upungufu wa wafanyakazi, vijana wengi wakitekwa na vileo ni kati ya hasara ninayoshuhudia chai ikikomaa shambani na kupita kiwango cha ubora unaotakikana.”

Mkulima huyo hata hivyo anaamini teknolojia, mifumo ya kisasa na bunifu kuendeleza kilimo zitavutia vijana wanaoshikilia kwamba zaraa ni kazi ya waliostaafu.

Mtambo huo unauzwa Sh30,000, mtumizi akitakiwa kuvalia miwani, vidude vya kupunguza sauti ya juu masikioni, glavu na gambuti.

Haipaswi kutumiwa wakati wa mvua.

Baadhi ya maeneo, mashine hiyo imezua mvutano wanaoipinga wakihoji itapunguza nafasi za kazi.

Chai, ni miongoni mwa mazao yanayoweka Kenya katika ramani ya ulimwengu.

  • Tags

You can share this post!

MITAMBO: Mseto wa mitambo 2 kuandaa lishe kamilifu

Mwezi mzima bila masomo katika JSS

T L