• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Mwingereza ataka jaji ajiondoe kwenye kesi ya ulezi wa mtoto

Mwingereza ataka jaji ajiondoe kwenye kesi ya ulezi wa mtoto

Na BRIAN OCHARO

MWANAMUME ambaye ni raia wa Uingereza, anataka jaji wa Mombasa ajiondoe kwenye kesi inayohusu mzozo wa ulezi wa mtoto kati yake na mwanamke Mkenya aliyekuwa mpenzi wake.

Raia huyo wa Uingereza amewasilisha kesi wiki moja baada ya kupoteza nafasi ya kumlea mtoto huyo. Mahakama ilimuagiza juma lililopita, kuwa amrudishe mtoto huyo wa kiume mwenye umri wa miaka mitatu kwa mama yake.

Mahakama pia iliagiza kuwa atakuwa na nafasi ya kumuona mtoto huyo.Jaji John Onyiego alitupilia mbali amri ya mahakama ya watoto ambayo ilikuwa imempatia Muingereza huyo ulezi wa mtoto huyo.

Mlalamishi sasa amewasilisha kesi akitaka Jaji Onyiego ajiondoe kwenye kesi hiyo akidai kuwa mapendeleo.Kupitia kwa mawakili wake Bi Pauline Wacu na Bw Laurence Obonyo, amemshutumu jaji huyo kwa kufanya maamuzi ambayo yanampendelea mwanamke huyo.

“Korti hii imefanya maamuzi kadhaa ambayo, licha ya ushahidi mwingi, yanampendelea mwanamke huyo. Ninahisi kuathiriwa na uamuzi wake wa kumpa mwanamke huyo mtoto bila kumfanyia uchunguzi wa akili,” alisema.

Raia huyo wa Uingereza pia amemwandikia barua Kaimu Jaji Mkuu Philomena Mwilu akilalamikia jinsi jaji huyo amekuwa akiendesha kesi hiyo.Katika barua hiyo, afisa huyo wa zamani wa Scotland Yard amelalamika kuwa jaji huyo amekuwa akipeana amri ambazo zinaweza kuhatarisha maisha ya mtoto huyo.

Mwanamke huyo alikuwa amekata rufaa kuhusu uamuzi wa korti ya watoto, ambayo ilimpatia fursa mwanaume huyo awe akimuona mtoto.Katika uamuzi huo, hakimu pia aliagiza mwanamke huyo kumpa Muingereza huyo vyeti vya kuzaliwa vya mtoto huyo ili kumwezesha kumsajili kama raia wa Uingereza na kumpatia hati ya kusafiria ya Jumuiya ya Ulaya ya Ireland.

Mwanamke huyo amepinga uamuzi huo, akidai kwamba korti ilimnyima ulezi wa mtoto wake licha ya ukweli kwamba bado ananyonyesha. Pia ameelezea hofu kwamba kitu kibaya zaidi kinaweza kumtokea mtoto huyo akiwa chini ya ulinzi wa mwanamume huyo, baada ya kumshauri kutoa mimba wakati wa ujauzito.

“Kuna hatari kuwa mtoto huyo anaweza kuondolewa humu nchini kwa sababu raia huyo anataka kuwa na hati zake za kuzaliwa,” aliiambia mahakama.

Hata hivyo, mwanamume huyo anasema kuwa juhudi za kumnyima kuona mtoto wake zinatokana na upotoshaji na kuficha kwa makusudi ukweli wa vitu kwa lengo moja tu la kupotosha korti kufikia uamuzi usiofaa.

“Ameshindwa kufichua ukweli wa mambo katika maombi yake. Haja yake ni kuninyima haki ya kuona mtoto wangu,” alisema.Pia amehimiza korti kutokubali kile anachosema ni mipango ya mwanamke huyo kuendelea kufaidika kutoka kwake.

Mwingereza huyo anadai kuwa afya ya mtoto itakuwa hatarini akiachwa chini ya ulinzi wa mwanamke huyo, ambaye anadai kuwa hana akili timamu.Amedai kuwa mwanamke huyo hawezi kuachwa kumtunza mtoto huyo kwa amefyeka pesa zote kwenye akaunti yake ya benki.

  • Tags

You can share this post!

Bei ya majanichai imepungua kwa asilimia 12 – KTDA

Shule za kibinafsi zalalamikia ubaguzi