• Nairobi
  • Last Updated June 1st, 2024 1:52 PM
Nataka nidhamu ya juu, Raila atetea kutimuliwa kwa waasi ODM

Nataka nidhamu ya juu, Raila atetea kutimuliwa kwa waasi ODM

Na GEORGE ODIWUOR 

Kiongozi wa ODM aliye pia kinara wa Azimio Raila Odinga ametetea hatua ya chama chake kutimua waasi kwa madai ya kushirikiana na serikali ya Kenya Kwanza.

Bw Odinga alisema uamuzi ambao chama kilichukua wa kuchuja viongozi hao ulikuwa wa busara.

Kulingana na Waziri Mkuu huyo wa zamani, kuna sheria zinazoendesha chama cha ODM na kwamba wanachama lazima wazifuate.

Alisema wanachama ambao wamechujwa walikiuka kanuni pale walipotangaza wazi kuunga mkono serikali ya Rais William Ruto.

Chama hicho mnamo Jumatano, Septemba 6, 2023 kilitimua wabunge kadhaa na kuwaambia wametolewa kwenye orodha ya wanachama.

Wabunge hao ni Elisha Odhiambo (Gem), Caroli Omondi (Suba Kusini), Gideon Ochanda (Bondo), Tom Ojienda (Seneta, Kisumu) na Mbunge wa Lang’ata Phelix Odiwuor.

Kulingana na Bw Odinga, haikuwa makosa kwa viongozi hao kukutana na Rais katika Ikulu.

Lakini akasema makosa waliyofanya ni kutoshauriana na chama kuhusu ziara yao hiyo Ikulu.

“Walidai kwamba wameenda Ikulu kutafuta maendeleo. Lakini ukweli ni kwamba walienda huko kwa maslahi yao ya kibinafsi,” akasema.

Viongozi hao waasi wamekuwa wakijitetea kwamba walienda kuonana na Rais kujadili jinsi maeneo yao yatapata maendeleo.

Lakini Bw Odinga amepuuzilia mbali kujitetea kwao akisema kwamba mipango yote ya maendeleo ina mwongozo kuhusu jinsi inatekelezwa.

“Mipango yote ya maendeleo lazima ipitie Bunge la Kitaifa,” akasema kiongozi huyo wa ODM.

Kinara huyo alishutumu wabunge hao kwa kuwa katika kikosi alichosema kinafifisha mafanikio ya muungano wa Azimio.

Alisema ili muungano usimame na kuwa thabiti, lazima chama cha ODM kiwe na watu ambao ni wakweli na wa kuaminika.

Alikuwa akizungumza Ijumaa, Septemba 8, 2023 katika uwanja wa Maranatha, mjini Migori wakati wa mkutano wa wajumbe. Alikuwa ameandamana na Gavana wa Migori Ochilo Ayacko, Seneta Eddy Muok, Mwanamke Mwakilishi Fatuma Mohamed, wabunge Peter Masara (Suna Mashariki), Tom Odege (Nyatike) na Walter Owino (Awendo).

Waziri wa zamani Eugene Wamalwa, na magavana wa zamani Mwangi wa Iria na Ndiritu Muriithi pia walikuweko.

Bw Odinga alisema yungali kwenye vita vya kisiasa na Rais Ruto na kwamba haelewi iweje wandani wake wafanye kazi na ‘adui’ yake.

“Chama chetu kinahitaki watu walio na nidhamu, walio na mapenzi ya dhati. Huwa tunasaidia walio na shida hivyo haieleweki ni nini hawa wanatafuta kwa serikali,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Mwanamume na wakwe wazozania maiti, mochari yasubiri mkwamo...

Watu 23 waangamia katika ajali tofauti barabara ya...

T L