• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Nyota ya Kawira Mwangaza yazidi kufifia, akikamatwa kwa kuhudhuria mkutano wa “Okolea”

Nyota ya Kawira Mwangaza yazidi kufifia, akikamatwa kwa kuhudhuria mkutano wa “Okolea”

Na DAVID MUCHUI

Kioja kimeshuhudiwa Jumatano Oktoba 18, 2023 eneo la Imenti ya Kati wakati Gavana Kawira Mwangaza alipokamatwa na kusukumwa kwenye karandinga la polisi kwa kile alichosema ni kusambaza ng’ombe wa maziwa katika kaunti hiyo.

Wakati wanahabari walipowasili, walimpata Bi Mwangaza akiwa kwenye karandinga la polisi katika mtaa wa Ruiga.

Inadawai kwamba gavana huyo alikamatwa kwa kuhudhuria mikutano yake ya “Okolea” ambayo ilipigwa marufuku na Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki.

Mwezi jana, mshikemshike pia ulishuhudiwa Igembe Kusini wakati Bi Mwangaza alipokuwa anaendesha mradi wake wa ‘Okolea’, ambapo watu kadhaa walijeruhiwa na ng’ombe aliokuwa agawanye kwa wakazi masikini kuchinjwa.

Tukio hili lilifanya Profesa Kindiki kupiga marufuku shughuli za mradi huo akisema umesababisha mgawanyiko miongoni mwa jamii ya Meru.

Mradi huo wa ‘Okolea’ unatumiwa na Bi Mwangaza kusambaza bidhaa kwa wasiojiweza.

Hata hivyo, saa kadhaa baada ya kukamatwa kwake, polisi bado hawajatoa taarifa kamili kuhusu tukio hilo.

Mnamo Jumanne Oktoba 17, 2023, madiwani wa Bunge la Kaunti ya Meru walikuwa wameanzisha tena jaribio la pili la kumng’oa mamlakani kiongozi huyo wa kaunti kwa misingi ya hoja saba.

Bunge la Kaunti hiyo lilifanya jaribio la kwanza la kumfurusha Gavana Mwangaza Disemba 14 mwaka jana kabla ya Seneti kutupilia mbali kufurushwa huko Disemba 30.

Lakini baada ya miezi kadhaa ya uhusiano wa joto-baridi, Kiongozi wa Wengi katika bunge hilo Evans Mawira aliwasilisha Jumanne asubuhi notisi ya kumng’oa mamlakani, na kumpa siku saba gavana huyo kujitetea.

Miongoni mwa mashtaka hayo ni madai ya ubadhirifu na utumizi mbaya wa pesa za kaunti, upendeleo, vitendo visivyo na heshima, dharau kwa viongozi wengine na uajiri usiofuata sheria.

 

  • Tags

You can share this post!

Watahiniwa pekee wasalia shuleni Riokindo, wanafunzi...

Taharuki punda zaidi ya 30 wakichinjwa Kitui na nyama...

T L