• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Taharuki punda zaidi ya 30 wakichinjwa Kitui na nyama kutoroshwa

Taharuki punda zaidi ya 30 wakichinjwa Kitui na nyama kutoroshwa

Na BONIFACE KANYALI

Hali ya mshikemshike imetanda katika Kaunti ya Kitui haswa maeneo ya Mwingi baada ya gari aina ya pickup kunaswa na polisi likisafirisha nyama na ngozi za punda zaidi ya kumi katika eneo la Kanyoonyoo, Kitui. 

La kuhofisha zaidi ni kuwa, huenda wakazi wa maeneo ya karibu na Mwingi wanaonunua nyama kwenye maeneo ya kuuzia nyama wakala nyama ya punda bila kujua, kwani hakuna tofauti ya nyama ya punda na wanyama wengine.

Nyama ya punda walionaswa inasemekana kutoka maeneo ya Nguutani eneobunge la Mwingi Magharibi na huenda ilikuwa inasafirishwa hadi Nairobi.

Hii imetokea siku chache baada ya nyama ya punda wengine kumi kuteketezwa an maafisa wa kijasusi mjini Mwingi. Takwimu za punda walioandikishwa kupotea katika maeneo ya Mwingi kwa sasa imefikia 38.

Akizungumza baada ya kushuhudia tukio la Jumanne Oktoba 17, 2023 katika Kituo Cha polisi Cha Kanyoonyoo, Waziri wa Kilimo katika Kaunti ya Kitui Mbaya Kimwele alikemea tukio hilo na kutoa onyo kali kwa wahalifu wanaoiba na kuchinja punda kuwa chuma chao ki motoni.

“Ningependa kutoa onyo kali kwa majangili wanaoiba punda, kuchinja na kuuza nyama yake kwa watu wasuojua. Tumeweka mikakati kama serikali ili kuhakikisha kuwa tabia hii mbovu imekomeshwa na wakulima wa Kitui wanaendelea kumtumia mnyama huyu kujinufaisha kimapato bila wasiwasi,” alionya Bw Kimwele.

Waziri huyo pia aliwataka maafisa wa polisi kuwachukulia hatua kali washukiwa wa ulanguzi wa nyama ya punda ili kukomesha wizi wa mnyama huyo Mwingi.

“Nawaomba maafisa wa polisi wawe makini zaidi na kuwatia mbaroni mara moja wahalifu wanaoiba na kuchinja punda kiholela,” alisema waziri huyo.

Ambrose Musyimi ambaye ni afisa anayefanya kazi na Kikundi cha kanisa katoliki Cha Caritas Kitui, na anayehusika na utetezi wa haki za punda amesema kuwa matukio ya hivi majuzi yamemhatarisha zaidi mnyama huyu.

Bw Musyimi alisema kuwa shirika la Caritas linafanya kazi kwa karibu na serikali ya Kaunti ya Kitui ili kuhakikisha kuwa Sheria madhubuti zinawekwa ili kumtunza punda kutokana na uhalifu.

“Mnyama kama punda ana faida kubwa akiwa hai kwani hutumika na wakazi wa Kitui kujitafutia pesa na pia kutekeleza kazi mbali mbali za kinyumbani,” alisisitiza Bw Musyimi.

Afisa huyo alisema kuwa kupitia kwa mradi wao wa ‘Mtunze Punda Daima’ shirika la Caritas Kitui linaendelea kuwaelimisha wakazi wa Kaunti ya Kitui kuhusu umuhimu wa punda na jinzi ya kumtunza ili kuwanufaisha zaidi.

Pia aliwaomba wakazi wa Kitui kuwa makini na kupiga ripoti kwa polisi wakishuku njama yoyote au kisa cha kuchinjwa kwa punda.

  • Tags

You can share this post!

Nyota ya Kawira Mwangaza yazidi kufifia, akikamatwa kwa...

Wanaume hutumia muda mwingi kuchakura mitandao, kushiriki...

T L