• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
‘Mizimu’ ya Shakahola yaandama mochari na hospitali ya Malindi

‘Mizimu’ ya Shakahola yaandama mochari na hospitali ya Malindi

NA FARHIYA HUSSEIN

VITENGO vya matibabu na mochari katika Hospitali Kuu ya Malindi vinakabiliwa na changamoto kubwa tangu miili ya walioondolewa kwenye makaburi ya Shakahola kuanza kupelekwa huko.

Mwezi wa Aprili, maiti zilizofukuliwa kutoka kutoka msitu wa Shakahola zilielekezwa katika mochari ya hospitali hiyo na kulingana na Msimamizi wa Matibabu wa Hospitali Kuu ya Malindi, Dkt David Mang’ong’o, jukumu hili ingawa ni muhimu, limesababisha ada kupungua na kufikia Sh550,000, na kuzidisha matatizo katika mfumo wa afya ambao tayari umeelemewa.

“Kabla ya mauaji ya Shakahola, tulikuwa tukikusanya Sh700,000 kila mwezi lakini sasa tunapata Sh150,000 kwa sababu ya msongamano wa maiti katika chumba cha kuhifadhia maiti,’ alisema Dkt Mang’ong’o.

Alibainisha licha ya chumba cha kuhifadhia maiti kubaki wazi na kufanya kazi, umma hupendelea kuhifadhi au kutuma miili ya jamaa zao katika vituo vingine.

“Kila wakati kuna mteja kutoka ndani ya hospitali au nje, hupendelea miili kupelekwa kwenye vyumba vya kuhifadhia maiti vya kibinafsi na vituo vingine,” Dkt Mang’ong’o alisema.

Aliongezea kuwa dhana ya watu wengi kutopendelea kuchanganya wapendwa wao karibu na pale chumba cha kuhifadhia maiti za Shakahola, imesababisha hospitali kuwa katika hali ya kusikitisha ada zinazowezesha shughuli za kila siku zikipungua.

Huku wateja wakizidi kuchagua kuhamisha mabaki na miili ya wapendwa wao kwenye vituo vingine, vikiwemo vyumba vya kuhifadhia maiti vya kibinafsi, hospitali haikabiliani tu na ufinyu wa kifedha bali pia na kazi ngumu ya kukidhi mahitaji ya afya ya jamii.

“Hospitali ya Malindi ina chumba cha kuhifadhia maiti cha ada nafuu zaidi katika eneo hili. Tukipewa nafasi ya kuhudumia jamii, tunaichukua kwa heshima na kuwahudumia watu ipasavyo. Lakini shughuli inayoshuhudiwa karibu na eneo la chumba cha kuhifadhia maiti imeonekana kuchangia pakubwa kwa hali hii ya kupungua kwa umma kutaka kutumia chumba hicho,” alisema Dkt Mang’ong’o

Kituo hicho kina uwezo wa kuhifadhi miili 30.

Mwezi wa Agosti, hospitali hiyo ilipokea kontena la pili litakalotumika kuhifadhi maiti zilizofukuliwa katika msitu wa Shakahola ili kupunguza msongamano katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali hiyo.

Hii ni baada ya usimamizi wa hospitali hiyo kuibua wasiwasi kuwa imekuwa ikipoteza kiwango cha ada inayopokea kutoka kwa wanajamii waliokuwa wakipeleka miili ya jamaa zao katika vituo tofauti.

Kontena hilo, lenye uwezo wa kuhifadhi miili 250 hadi 300, lilitolewa na Shirika la Msalaba Mwekundu Nchini baada ya kontena la kwanza kusemekana kutotosha.

Wiki moja iliyopita, maafisa wa upelelezi walikumbana na maiti iliyooza katika msitu wa Shakahola na kufikisha idadi ya waliofariki kuwa 429.

  • Tags

You can share this post!

Worldcoin iliingiza Sh2.5 bilioni nchini bila ufahamu wa...

ODM yaambia Jalang’o, waasi wenzake wakanyage nje

T L