• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
Omar Lali mpenziwe marehemu Tecra Muigai aagizwa ahudhurie vikao vya Kortini hadi uchunguzi wa kifo chake Tecra ukamilike

Omar Lali mpenziwe marehemu Tecra Muigai aagizwa ahudhurie vikao vya Kortini hadi uchunguzi wa kifo chake Tecra ukamilike

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA ya Milimani Jumatano ilimwamuru Omari Lali ahudhurie vikao vyote vya kutoa ushahidi kuhusu kifo cha aliyekuwa mpenziwe Tecra Muigai.

Baada ya mashahidi wengine saba kutoa ushahidi Bw Lali ndipo ataingia kizimbani kujitetea dhidi ya madai ndiye alimuua Tecra..Hakimu mwandamizi Bi Zainab Abdul alitoa agizo hilo baada ya Bw Lali kutiwa nguvuni na polisi kutoka Lamu na kusafirishwa hadi Nairobi Jumatatu kuhudhuria vikao vya uchunguzi wa kutathmini kilichosababisha kifo cha Tecra.

“Ushahidi unaotolewa mbele ya korti unakuhusisha na kifo cha Tecra mliyekuwa naye usiku wa Aprili 22/23, 2020 alipoumia na hatimaye akaaga.Utakaa hapa kortini kuwasikiza mashahidi wote kabla ya kuwekwa  kizimbani kujitetea,” Bi Abdul alimwamuru Bw Lali.

Bw Lali aliyekamatwa na kuachiliwa kwa maagizo ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Nordin Haji ili mahakama ichunguze kifo cha Tecra ndiye mshukiwa mkuu.Madaktari watano Dkt Bakar Mohamed Bakar, Prof Emily Rogena, Dkt Esther Matu, Dkt Johansen Oduor na Dkt Andrew Kanyi Gachii waliofika kortini walisema “kifo cha Tecra kilitokana na majeraha ya ubongo yaliyosababishwa na kichapo na kifaa butu.”

Alipompeleka Tecra kutibiwa katika Zahanati iliyoko eneo la Shella na hatimaye katika hospitali ya King Fahad,Bw Lali aliwaeleza mpenziwe huyo aliteleza kwenye ngazi za jumba lao la kifahari na kugonga ukuta.Watu wa familia ya Bw Lali waliofika kumpeleka hospitali alfajiri ya Aprili 23, 2020 walieleza mahakama marehemu alikuwa anavunja damu kutoka sikio lake  la upande wa kushoto.

Bw Ali Bakar Mohamed (kati), shemejiye Lali…Picha/RICHARD MUNGUTI

Nduguye Lali , Bw Quswali Lali ambaye ni seremala alieleza mahakama alipokea simu mwendo wa saa kumi na mbili kasorobo kutoka kwa nduguye (lali) akimtaka afike kwake amsaidie kumpeleka Tecra hospitali.Tecra alikuwa ameumia.

“Nilipofika kwa Lali nilibisha kisha akanifungulia. Nilimpata Tecra amelala sakafuni akivunja damu kutoka sikio la kushoto,” alisema Quswali.Shahidi huyo alimweleza  hakimu Tecra na nduguye walikuwa “wapenzi wa chanda na pete na hakuwahi kushuhudia wakizozana.”

Quswali aliyehojiwa na wakili Abubakar Yussuf, alisema , “Tecra alikuwa mkarimu, machangamfu na alikuwa amempenda Mama yetu.Akija nyumbani alikuwa anawachukua watoto wetu kwenda kuwatembea nao.”Akaongeza kusema, “Tecra alikuwa ameapa ataishi nasi maisha yake yote.”

Shemejiye Bw Lali ambaye ni Nahodha wa meli za kutembeza watalii bahari Hindi na mlinzi katika afisi za kaunti ya Lamu, Bw Ali Bakari Mohamed walipasua kilio kortini alipotoa ushahidiBw Mohamed anayetoka eneo la Shella viswani Lamu alianza kulia aliposimulia jinsi walivyompeleka Tecra hospitali alipoumia na hatimaye akafahamishwa alifariki akipata matibabu katika Nairobi Hospital Mei 2020.

Ilibidi hakimu asimamishe kesi kwa muda wa dakika kumi ili Bw Mohamed atulie.Bw Mohamed alimweleza hakimu ,” singelipenda msichana yeyote afe ama kudhulumiwa kwa njia yoyote ile. Mimi nimebarikiwa kuzaa wasichana wanne na ninapomkumbuka Tecra huzuni hunikera.”

Shahidi huyo alieleza hakimu alimpeleka hospitali ya Shella na King Fahad.Alisema Tecra na Lali walikodisha meli yake akawatembeza bahari Hindi kwa siku sita kwa bei ya Sh60,000.“Kutokana na furaha aliyopata Tecra alinialika mimi na watu wengine watatu wa familia yetu kuzuru kwao Naivasha,” alikumbuka Bw Mohamed.

Alisema walikaa Naivasha siku nne mnamo 2019 kisha wakaabiri ndege hadi kisiwani Lamu.Alianza kulia kisha Bw Lali naye akaanza kulia.“Tulia. Mambo sio rahisi.Sisi wote tuko na hisia kuhusu kisa hiki,” wakili Elisha Ongoya anayewakilisha familia ya Tecra alimweleza.

Bw Mohamed alisema Bw Lali alipofika katika Jaha House alipokuwa akiishi na Tecra alimpata amemshika Tecra.“Nilirudi kwa nyumba kuchukua viti viwili vya Plastic Tecra akalie tukimpeleka hospital.“Je uliona akivuja damu,” kiongozi wa mashtaka alimwuliza Mohamed.

“Hapana ila niliona maji sakafuni. Sikujua ni mkojo ama ni maji yapi.Tecra alikuwa amelewa chakari,” Mohammed alisema.Bw Abdul Hakim, nduguye Lali , alisema polisi walimkabidhi vifunguo vya jumba Jaha House ambapo Lali na Tecra walikuwa wakiishi.

“Polisi walinipa funguo za nyumba baada ya kumkamata Omar,” Hakim alimweleza.Hakim ni meneja wa hoteli moja visiwani Lamu. Alisema mara kwa mara Tecra na Omar walikuwa wakienda kujivinjari na kujistarehesha.Madaktari Johansen Oduor na Dkt  Andrew Kanyi Gachii waliotoa ushahidi walisema kifo cha Tecra kilitokana na majeraha ya ubogo.

Dkt Gachii alionyesha akitumia sanamu ya kichwa jinsi Tecra alivyokuwa ameumia. Alihojiwa na wakili James Orengo anayewakilisha familia ya Tecra katika uchunguzi huo.

Kesi inaendelea kusikizwa..

  • Tags

You can share this post!

Shujaa yafunzwa umuhimu wa utimamu wa kiakili nao Lionesses...

Siri kali ya Joho, Waiguru