• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Pasta adaiwa kuua mkewe na kutuma mwanawe kumfahamisha chifu

Pasta adaiwa kuua mkewe na kutuma mwanawe kumfahamisha chifu

NA VITALIS KIMUTAI

POLISI katika Kaunti ya Kericho wanamzuilia pasta mmoja eneo hilo anayeshukiwa kumuua mkewe kufuatia mzozo wa kinyumbani.

Katika kisa cha kikatili ambacho kimeshtua wakazi, pasta huyo mwenye umri wa miaka 35 katika kanisa la Holistic Church, alimtuma mwanawe kwa mzee wa kijiji ili amfahamishe kuhusu kitendo hicho.

Inashukiwa kuwa pasta huyo alimpiga mara kadhaa mkewe mwenye umri wa miaka 32 kwa kipande cha kuni baada ya kugombana wakiwa nyumbani kwao kijiji cha Burgei, eneobunge la Kipkelion Mashariki.

Chifu wa kata ya Kedowa, Bw John Ngetich aliyethibitisha kisa hicho, alisema kwamba pasta huyo pia alimkata mwanamke huyo kwa upanga shingoni.

Bw Ngetich alisema kwamba baada ya kumuua mkewe, mshukiwa ambaye ni baba wa watoto sita, alifunika mwili kitandani na kukesha sebuleni.

“Mnamo Jumatano asubuhi, alimwamsha mwanawe kifungua mimba na kumtuma kwa mzee wa kijiji, kumweleza alikuwa amemjeruhi vibaya mkewe na hakuwa amemshughulikia. Alimweleza mwanawe kumwambia mzee wa kijiji kuhusu mauaji hayo ya kikatili,” alifichua Bw Ngetich.

Mzee wa kijiji alipofika, pasta huyo alimwambia aingie katika chumba cha kulala kuangalia hali ya mwathiriwa.

Ni wakati huo ambapo mzee wa kijiji aligundua kwamba mwanamke huyo ambaye ni mfanyabiashara katika kituo cha kibiashara cha Chepseon alikuwa amekufa huku mwili wake ukiwa umelowa damu.

Chifu huyo aliwaita polisi ambao walifika na kumkamata mshukiwa. Mwili wa mwathiriwa ulipelekwa katika mochari ya hospitali ndogo ya Londiani.

Mshukiwa anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Londiani huku uchunguzi kuhusu tukio hilo ukiendelea.

Inadaiwa kuwa mwezi Januari 2023, pasta huyo alionya kuwa angemuua mkewe kufuatia mzozo wa kinyumani kati yao.

“Tulimshauri asichukue hatua kama hiyo, lakini wazungumze na tukadhani alikuwa amezingatia ushauri wetu. Tumeshtuka kwamba kweli amemuua mkewe,” alisema mwanakijiji ambaye aliomba asitajwe jina.

  • Tags

You can share this post!

Pasta Ezekiel ataka serikali ikome kumhusisha na Mackenzie

Fraser-Pryce, Mkenya Imali kukabiliana Kip Keino Classic

T L