• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Poleni sana lakini tutapandisha nauli, wamiliki wa matatu wasema

Poleni sana lakini tutapandisha nauli, wamiliki wa matatu wasema

Na WINNIE ATIENO

WAMILIKI wa Matatu Nchini Kenya wamemtaka Rais William Ruto kuchunguza ruzuku ya mafuta ya petroli ili kuokoa maisha ya Wakenya ambao wanaendelea kuhangaika kutokana bei ghali ya mafuta inayoendelea kuongezeka kila kuchao.

Agosti mwaka huu, serikali ya Kenya Kwanza ilirejesha ruzuku iliyokuwa imewekwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta wakati alipokuwa mamlakani ili kuokoa maisha ya Wakenya kutokana na gharama ya mafuta.

Hata hivyo, licha ya kurejeshwa kwa ruzuku hiyo, bei ya mafuta imekuwa ikiendelea kupanda na kuzidi Sh200.

Mwenyekiti wa Kitaifa wa Wamiliki wa Matatu, Bw Albert Karakacha, alisema licha ya kurejeshwa kwa ruzuku ya mafuta, gharama ya mafuta imekuwa ikiongezeka.

Alisema wamiliki hao watalazimika kuongeza bei ya nauli kufuatia kuongezeka kwa bei ya mafuta.

“Inashangaza kuwa bei inazidi kupanda licha ya ruzuku ndio maana tunamsihi Rais Ruto kuchunguza na kuweka mikakati mipya ya kusaidia Wakenya ambao wanaendelea kuhangaika kutokana na gharama ya juu ya maisha,” alisema.

Akiongea kwenye mkutano na washika dau wa sekta ya uchukuzi katika hoteli ya Darajani, mjini Mombasa, Bw Karakacha, alisema bei ya mafuta inapoendelea kuongezeka, abiria na wamiliki wa magari ya umma wanaendelea kugharimika.

Alisema baada ya Halmashauri ya Kawi kuongeza bei ya mafuta, wamiliki wa matatu walilazimika kuongeza nauli.

Bw Karakacha alisema RaisRuto hana budi ila kuokoa Wakenya wanaohangaika baada ya kuwaahidi wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka jana.

“Hali imekuwa ngumu, Wakenya wanahangaika. Rais Ruto, hawa ni raia ambao uliapa kuwa utawapa kipaumbele utakapoingia mamlakani. Tunakusihi uokoe Wakenya, vile vile tunawaomba Wakenya watuwie radhi sababu tumelazimika kuongeza bei ya nauli,” alisema.

Wakati huo huo, muungano huo umeitaka serikali kukabiliana na ufisadi katika Mamlaka ya Kudhibiti Usalama Barabarani (NTSA).
Bw Karakacha aliitaka NTSA kukabiliana na kampuni na sacco zinazosimamia matatu katika maswala ya usalama barabarani badala ya kufuata wamiliki wa magari hayo ya umma.

Alisema magari hayo ya umma yanasimamiwa na sacco.

Aliongeza kuwa washikadau wa sekta hiyo wanakabiliwa na hali ngumu, hasa kutokana na misako ya mara kwa mara inayoendeshwa na NTSA.

Alilaumu ufisadi barabarani kwa kuchangia katika ajali za mara kwa mara.

  • Tags

You can share this post!

Wananchi wa Oman, Yemen na Saudi Arabia kuanza kunywa...

Karen Nyamu atishia kuchochea wanawake Nairobi kuvua nguo...

T L