• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Wananchi wa Oman, Yemen na Saudi Arabia kuanza kunywa maziwa ya Fresha kutoka Githunguri

Wananchi wa Oman, Yemen na Saudi Arabia kuanza kunywa maziwa ya Fresha kutoka Githunguri

NA LABAAN SHABAAN

USHIRIKA wa Wafugaji wa Ng’ombe wa Maziwa wa Githunguri utauza maziwa lita 250, 000 kila mwezi hadi Bara Asia

Wananchi wa mataifa ya Oman, Yemen na Saudi Arabia watakata kiu yao ya maziwa kutumia maziwa ya ‘Fresha.’

Mwenyekiti wa ushirika huo, George Kinuthia, alisema wameanza kusambaza maziwa ya kiwango cha lita 113,750.

Akizungumza katika mkutano mkuu wa mwaka katika Uga wa Githunguri, Bw Kinuthia amedokeza mauzo yataongezeka kadri soko la kimataifa linavyokua.

“Kuna uhaba wa maziwa si Kenya tu bali pia kote duniani. Sisi kama mmoja wa wazalishaji wakubwa wa maziwa nchini, tunafurahia kunasa soko la kimataifa,” alisema Bw Njoroge akiamini wakulima watakua kiuchumi.

“Tunajua kuwa maziwa ya Kenya yanafanya vizuri katika soko la kimataifa. Ni wakati serikali na washikadau wanafaa kuimarisha juhudi ili kustawisha sekta ya maziwa kuuza maziwa nje,” aliongeza.

Ripoti ya fedha ya mwaka wa 2022/2023 inaonyesha ushirika huu umeongeza mapato kutoka Sh9.2 bilioni hadi Sh9.9 bilioni.

Kadhalika, ripoti hii imenakili kuwa, kufikia Juni 30, 2023, thamani ya mali ya ushirika imekua hadi Sh3.14 bilioni kutoka Sh2.95 bilioni ndani ya mwaka mmoja.

“Mtaji wetu wa hisa umepanda kutoka Sh589.1 milioni hadi Sh607,9 milioni huku kipato cha mapato cha wanachama kikishuka kutoka Sh175.4 milioni hadi Sh158.2 milioni. Hii ni kwa sababu ya gharama ya biashara kuathiriwa na gharama ya juu ya maisha,” mwenyekiti alikiri.

Kwa mujibu wa rekodi ya mwaka huu, uanachama wa ushirika umekua kutoka wanachama  27,113 hadi 27,607 na kuzidisha kiwango cha maziwa kwa mwaka.

  • Tags

You can share this post!

Jaji Mkuu Martha Koome afika Bungeni kushauriana na Spika...

Poleni sana lakini tutapandisha nauli, wamiliki wa matatu...

T L