• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 9:50 AM
Polisi wanasa lori likipeleka paka 1,000 kichinjioni

Polisi wanasa lori likipeleka paka 1,000 kichinjioni

NA MERCY KOSKEI

POLISI nchini China wamewaokoa paka 1,000 kutoka kwa lori lililokuwa likielekea kwenye kichinjio kimojawapo nchini humo.

Hii ni baada ya maafisa kutoka Zhangjiagang, katika jimbo la mashariki la China la Jiangsu, kudokezewa na wanaharakati wa kuwalinda wanyama kwamba kulikuwa na njama fiche.

Kulingana na gazeti la serikali la The Paper, maafisa hao walinasa gari hilo lililokuwa likitumika kukusanya na kusafirisha paka hao bila idhini.

Wanaharakati hao waliliripoti kuwa waliona idadi kubwa ya masanduku ya mbao yaliyotundikwa huku ndani kukiwa na paka wengi.

Walipiga doria mitaani kwa siku sita kabla ya lori hilo kuwasafirisha paka hao hadi kichinjioni, waliingilia kati na kuwaita polisi.

The Paper lilidokeza kuwa hii ni sehemu ya biashara haramu ambayo matokeo yake ni watu kuuziwa nyama ya paka hivyo kuzua wasiwasi wa usalama wa chakula.

Ripoti hiyo ilisema kuwa kundi hilo lilikuwa linapania kuchinja na kusafirisha paka hao kusini mwa China ili kutumiwa kama mishikaki ya nguruwe na kondoo pamoja na soseji.

Hata hivyo, lilibaini kuwa polisi na mamlaka ya kilimo baada ya kunasa paka hao walipelekwa kwa makazi salama na kuzuia biashara ambayo wahalifu wangepata dola 20,500 ambazo ni sawa na Sh3 milioni za Kenya.

Ripoti hiyo haikutaja ikiwa kuna washukiwa waliokamatwa, au kama paka walikuwa wamepotea au walikuwa wanyama pendwa wa kufugwa nyumbani.

  • Tags

You can share this post!

Tuonyeshe manufaa ya ziara chungu nzima za Rais Ruto,...

Kansa: Mwanamke asimulia jinsi mume alivyomuacha kwa...

T L