• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Tuonyeshe manufaa ya ziara chungu nzima za Rais Ruto, Wakenya mitandaoni wamuambia Seneta Cherargei

Tuonyeshe manufaa ya ziara chungu nzima za Rais Ruto, Wakenya mitandaoni wamuambia Seneta Cherargei

WANGU KANURI

WAKENYA mitandaoni wamemtaka Seneta wa Nandi Samson Cherargei kuorodhesha manufaa ambayo Rais William Ruto ameleta baada ya ziara zake nje ya nchi.

Hii ni baada ya gazeti la Taifa Leo kuchapisha orodha ya nchi ambazo Rais Ruto amezuru mwaka mmoja baada ya kushika hatamu huku wakilinganisha na marais waliomtangulia.

Taarifa hiyo iliibua hisia mseto, huku Seneta Cherargei kwa mfano, akikasirishwa vikali na taarifa hiyo na kudai kuwa nchi imeimarika kutokana na ziara zake Rais Ruto.

Hata hivyo, Wakenya walitilia shaka ripoti yake seneta huyo huku wakimtaka aorodheshe manufaa angalau machache ambayo Wakenya wamepata baada ya ziara hizo.

Walisema;

“Hizo ni likizo tu. Hakuna manufaa yoyote kwa Wakenya,” akaandika Joseph Njoroge.

“Mbona inakuwasha basi?” akauliza Isaac Otwona.

“Tuelimishe,” akasema Ubo Galugalu.

“Seneta, licha ya ushindi wenu mambo yanaweza kugeuka uchaguzi ujao. Kuweni na hisani,” akaandika James.

“Wanaopata manufaa ya ziara zake ni ndugu, jamaa na marafiki wake wa karibu kama wewe. Wakenya wengine wote wanaumizwa tu na gharama ya juu ya maisha na utozwaji ushuru kwa mishahara yao,” akasema Calvoh Okinyo.

“Tutajie manufaa matatu peke yake ambayo yametokana na kuharibu ushuru wa mwananchi kwa ziara za nje,” akaandika Mkenya Andez.

“Iwapo ungejua hasara inayotokana na ziara hizo hungepiga kelele mitandaoni. Kibaki hakuzuru kama yeye na sote tunajua alichofanya. Wewe unapenda kujipendekeza sana. Nyamaza sasa,” akasema Eng Geoffrey.

“Anaharibu tu pesa za wananchi,” akaandika Abala Kinyua.

“Manufaa sufuri,” akajibu Wycliffe Mwaka.

Uchunguzi wa gazeti hilo ulionyesha kuwa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta alifanya ziara 13 za nje katika mwaka wake wa kwanza afisini kati ya Machi 2013 hadi Machi 2014 ambazo ziligharimu mlipa ushuru Sh1.56 bilioni.

Hayati Mwai Kibaki alifanya jumla ya ziara 33 peke katika mataifa ya kigeni katika kipindi cha miaka 10 aliyoongoza kama Rais. Ukilinganisha, Rais Ruto alifanya ziara 11 kutoka Septemba 13, 2022, alipoingia Ikulu hadi Desemba 2022.

  • Tags

You can share this post!

Wakulima wa mashamba madogo waanza kukumbatia kilimo cha...

Polisi wanasa lori likipeleka paka 1,000 kichinjioni

T L