• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Kansa: Mwanamke asimulia jinsi mume alivyomuacha kwa kukatwa titi

Kansa: Mwanamke asimulia jinsi mume alivyomuacha kwa kukatwa titi

NA KALUME KAZUNGU

BI Shumi Abdallah Bakari ni miongoni mwa manusura wa maradhi ya saratani ya matiti kisiwani Lamu.

Mama huyo wa miaka 63 alipatikana akiugua ugonjwa huo mwaka 2013, wakati huo akiwa na umri wa miaka 53.

Yeye ni mzawa wa nchi jirani ya Tanzania lakini akiwa angali mdogo, mamake mzazi alihamia Kenya, hasa mtaa wa Mkomani kisiwani Lamu, ambapo Bi Abdallah alikulia, kuolewa na hata kuishi eneo hilo hadi sasa.

Bi Abdallah anakumbuka jinsi taarifa ya kuugua maradhi ya kansa ilivyomshtua na kumwacha hoi, japo alijitambua na kujikubali baadaye, hivyo kujipa moyo.

Kwa sasa yeye ni mwingi wa matumaini, akijifariji na kumuomba Mola kila kukicha azidi kusonga mbele.

Akielezea safari yake ya maisha, maradhi ya saratani na jinsi alivyojizatiti kutafuta tiba kwa udi na uvumba hadi kupona kwake, Bi Abdallah anasema alianza kujishuku siku moja pale alipokuwa amelala chali chumbani.

Alianza kukagua matiti yake na kisha kuhisi uvimbe usio wa kawaida na ambao hauna uchungu wala maumivu yoyote kwenye titi lake la kushoto.

Anasema punde alipogundua uvimbe huo, alimfuata mmoja wa mashemeji zake wa kike ambaye ni mhudumu wa afya na kumdokolea alilong’amua kwa titi lake.

Akashauriwa kutotia hofu na badala yake atembelee hospitali ili kukaguliwa na kupimwa dhidi ya maradhi ya saratani ya matiti.

Ikumbukwe kuwa saratani ya matiti ni mabadiliko ya chembechembe hai zilizopo kwenye matiti.

Saratani hii kwa kawaida haina dalili katika hatua za mwanzo.

Wanawake katika hatua za mwanzo za ugonjwa huwa hawana maumivu au dalili nyingine zozote.

“Niliposhauriwa kutembelea hospitalini, nilifunga safari kutoka Lamu hadi kwenye hospitali kuu ya Pwani-Makadara iliyoko mjini Mombasa. Lamu hatuna kituo chochote cha kukagua na kutibu saratani. Kwenye hospitali ya Mombasa-Makadara, nilipimwa na kupatikana kweli niko na kivimbe katika titi langu la kushoto. Nikashauriwa kufanyiwa upasuaji kuondoa uvimbe huo. Kwa sababu hospitali ya Makadara haikuwa na vifaa vya kutekelezea tiba hiyo, nikatafuta matibabu kwenye hospitali moja ya kibinafsi mumo humo mjini Mombasa. Upasuaji ukafaulu kufanyika, ambapo kivimbe kilitolewa salama,” akasema Bi Abdallah.

Anaeleza kuwa baada ya upasuaji, madaktari walitekeleza vipimo na ukaguzi zaidi, ambapo walimpata akiwa na kansa, japo ya awamu ya sufuri (Stage 0).

“Nilipoambiwa hilo nilishtuka na nikajiambia mimi kwisha. Baadaye nilijipa moyo nikijua fika kuwa saratani siyo mwisho wa maisha. Familia, ndugu, dada, jamaa na marafiki wangu wakaja pamoja na kunichangia fedha nyingi. Nilisafiri nchini Tanzania katika taasisi ya Matibabu ya Kansa ya Ocean Road iliyoko jijini Dar es Salaam. Kule nilikaguliwa tena na kuthibitishiwa kwamba ni kweli nilikuwa na kansa ya matiti, hivyo nilitakiwa kufanyiwa matibabu haraka iwezekanavyo kuzuia uwezekano wa maradhi hayo kusambaa kwenye viungo vingine,” akasema Bi Abdallah.

Tiba iliyopendekezwa na madaktari wake ni kukatwa titi lake la kushoto ili kupunguza au kukomesha kabisa msambao wa saratani mwilini mwake.

 “Kwa sababu nilitaka sana kuishi, nikachagua kwamba titi langu likatwe. Upasuaji ukafanywa na hivyo ndivyo nilivyopoteza kiungo hicho. Kisha nikapewa dawa za miaka mitano kutumia. Nikafuata masharti ya madaktari na wataalamu wengine wa matitabu. Nikameza dawa inavyostahili. Mwishowe nikaambiwa saratani mwilini mwangu imepotea. Ni mwaka wa saba sasa tangu nipone saratani ya matiti,” akasema Bi Abdallah.

Kinachomfanya kuchukia zaidi saratani na kuiwekea kinyongo au kisasi cha maisha ni jinsi ilivyobadili ghafla maisha yake.

Bi Abdallah alikuwa mkulima na mfanyibiashara tajika kisiwani Lamu.

Anasema kwa sasa hajaweza kurejelea kazi zake kwani anachunga zaidi afya yake na kujiepusha na jazba zozote za maisha, ikiwemo kazi ngumu na msongo wa mawazo.

Aidha kinachomuudhi na kumkeketa maini zaidi kuhusu kansa ni jinsi gonjwa hilo lilivyompokonya titi, kumfurushia mumewe na kuisambaratisha ndoa yake ya miaka kumi.

“Awali, mume wangu alikuwa akinisaidia kwa hali na mali. Alikuwa akinitumia fedha na kunifariji kisaikolojia. Punde nilipomjulisha kwamba matibabu yalifikia kiwango cha mimi kukatwa titi langu la kushoto, mume wangu wa miaka kumi hakuridhishwa na hilo. Aliniuliza mara mbilimbili na kisha kukata simu. Wakati huo hata nilikuwa bado niko nchini Tanzania. Hivyo ndivyo ulikuwa mwisho wake kujihusisha na mimi kwa jambo lolote. Alisusia kunipigia simu na kunisaidia kifedha kama zamani,” akasema Bi Abdallah.

Bi Shumi Abdallah Bakari,63, mkazi wa kisiwa cha Lamu, ambaye alitorokwa na mumewe wa miaka kumi punde alipogundulika kuugua maradhi ya saratani ya matiti, hali iliyosababisha yeye kukatwa titi lake la upande wa kushoto. PICHA | KALUME KAZUNGU

Anasema baada ya kurudi Lamu na kuona kimya cha mumewe kimezidi, Bi Abdallah aliamua kumpigia simu na kumuuliza kulikoni.

“Mume wangu alipasua mbarika kwamba alitaka kunitaliki. Hata hakujali angalau kuja kutazama lile kovu la titi langu lililokatwa kwa sababu ya kansa. Alipodai talaka sikumzuia kwani nilijua fika kuwa hajaridhishwa na kuugua kwangu saratani na hata kukatwa titi. Akanitaliki,” akasema Bi Abdallah.

Anaeleza kuwa kabla ya kuugua na kupona maradhi ya saratani, mumewe alikuwa na mapenzi tele kwake.

“Tulikuwa tumeaoana na kuishi kwa zaidi ya miaka kumi. Ni jambo linalonihuzunisha maishani kila nikitafakari jinsi saratani ilivyonipokonya bwanangu na titi langu. Hata hivyo nilijikubali na kubadili mwelekeo wangu wa maisha, nikitazama mbele zaidi jinsi nitakavyoiboresha aushi yangu jinsi miaka inavyosonga,” akasema Bi Abdallah.

Anawashauri wanawake kwa wanaume kujilinda na saratani ya matiti kupitia mja kujichunguza mwenyewe mara kwa mara, kufuatilia uchunguzi wa kitabibu wa matiti kila mwaka, uchunguzi wa matiti kwa njia ya mashine ya mionzi angalau mara moja kwa mwaka, hasa kwa waja wenye miaka zaidi ya 40.

Pia anawapa wosia wanawake wote wenye umri kuanzia miaka 21 kwenda juu wajichunguze matiti yao siku ya 5-7 baada ya kumaliza hedhi mbele ya kioo.

“Kuna hatua rahisi watu, hasa wanawake, wsnaweza kujichunguza matiti. Jitazame katika kioo ukiwa umesimama wima na umeweka mikono kiunoni. Hapa, utaangalia kama kuna mabadiliko katika umbo au rangi ya ngozi ya titi. Pia ukiwa umesimama au umelala chali, tumia mkono pamoja na kipaji cha vidole vya mkono wa kulia kuchunguza titi la kushoto na mkono wa kushoto kuchunguza titi la kulia kwa njia ya mzunguko. Kwa upole, pia waweza kukamua chuchu ya kila titi na kuchunguza kama kuna ute uliochanganyika na damu. Pia tudumishe mazoea ya kumuona daktari kama kuna uvimbe au ute ulio changanyika na damu au hali yoyote ulioiona wakati wa kujichunguza na ambayo wahisi si ya kawaida,” akasema Bi Abdallah.

Kauli yake ya mwisho kwa watu na jamii kwa ujumla ni kutowapuuza, kutowabagua au kuwatelekeza wanaougua na hata kupona maradhi ya saratani.

  • Tags

You can share this post!

Polisi wanasa lori likipeleka paka 1,000 kichinjioni

Shilingi ya Kenya ilidorora enzi za Uhuru lakini ikatiwa...

T L