• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
Pombe ya makore yatia doa Lamu, walevi wakigeuza vichaka lojing’i za uzinzi

Pombe ya makore yatia doa Lamu, walevi wakigeuza vichaka lojing’i za uzinzi

NA KALUME KAZUNGU

TANGU jadi, unaposikia jina ‘Lamu’ mara nyingi taswira inayojichora akilini ni tabia nzuri, nidhamu, uswalihina na unyenyekevu wa kidini.

Ikumbukwe kuwa Lamu ni eneo lililobeba historia kubwa, hasa kuhusiana na chimbuko la dini ya Kiislamu Pwani, Kenya na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Kwa karne na karne, Lamu inatambulika kuwa kitovu cha Uislamu.

Aidha miaka ya hivi punde, hali imeanza kubadilika kwani mtagusano wa watu au makabila tofauti, kutoka pande zote za nchi na ulimwenguni kote, kumeletea eneo hilo sifa nzuri na pia kwa upande mwingine sifa mbaya.

Sehemu mojawapo ya kijiji ca Manda-Maweni kilichoko katika Kaunti ya Lamu ambapo pombe ya makore imewasukuma walevi kugeuza vichaka kuwa lojing’i za uzinzi. PICHA | KALUME KAZUNGU

Miongoni mwa sifa mbaya zinazotia doa jeusi Lamu ni kukithiri kwa dawa za kulevya na ulevi kupindukia, hasa ule wa pombe ya kienyeji.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo ulibaini kuwa baadhi ya miji kama vile Manda-Maweni, Mararani, mitaa ya Hindi, Mpeketoni, Kibaoni na kwingineko imeathiriwa pakubwa na pombe na ulevi kupindukia.

Miongoni mwa pombe inayotumika sana na kuwafanya wanaume kwa wanawake kukosa kuwajibika ni ile ya makoremkoma na mnazi.

Katika kijiji cha Manda-Maweni, pombe ya makore imewasukuma walevi kugeuza vichaka na misitu kuwa lojing’i, hali ambayo inatia hofu jamii kuhusiana na mwelekeo wa kizazi kijacho eneo hilo.

Katika mahojiano na Taifa Leo Ijumaa, Mwanaharakati wa Kijamii katika kijiji cha Manda-Maweni, Ben Juma Ojuok alisema pombe ya makore imeleta athari kubwa kwa jamii inayoishi Manda-Maweni, akitaja kuwa vijana wengi wa kati ya umri wa miaka 13 hadi 23 tayari wameacha shule na kujitosa katika ulevi chakari wa pombe hiyo.

Bw Ojuok anasema cha kusikitisha zaidi ni kwamba vichaka vya karibu kila jua lituapo vinageuzwa kuwa maeneo ya wanawake na wanaume kufanya ngono.

Alieleza wasiwasi wake kuwa endapo hali hiyo haitadhibitiwa, jamii ya Manda-Maweni itaangamia kutokana na maradhi ya zinaa.

“Ulevi umekithiri Manda-Maweni. Cha kuudhi ni kwamba hawa walevi baada ya kulewa hugeuza vichaka kuwa lojing’i za kufanyia ngono. Hawafikirii hata kutumia kinga wanapofanya mambo yao ya uzinzi. Haya machimbo ya mawe pia mara nyingine wanayageuza kuwa malazi yao kuendeleza tabia hizo,” akasema Bw Ojuok.

Afisa huyo, ambaye pia ni Mwanzilishi wa Shirika la kutetea haki za watoto la Manda-Maweni Childcare Initiative (MMCI), alisema ulevi pia umechangia pakubwa wazazi kuwatelekeza watoto wao na kuwaacha kuhangaika ilhali wao wakizama kwenye pombe ya makore.

Mwanaharakati wa Kijamii na Mtetezi wa Watoto ambaye ni Mwanzilishi wa Manda-Maweni Childcare Initiative (MMCI) Bw Ben Juma Ojuok akipiga simu. Anasema walevi wanaobugia pombe aina ya makore kijijini Manda-Maweni wameingia kwa matatizo makubwa na ulevi huo umechangia idadi kubwa ya watoto wanaotelekezwa na wazazi wao. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Ojuok pia alieleza masikitiko yake kuhusiana na idadi kubwa ya wanafunzi walioacha shule na kuingilia ulevi na dawa za kulevya kijijini Manda-Maweni.

“Inasikitisha kuwa vijana wadogo wanaacha masomo na kuingilia ulevi wa pombe ya makore na dawa za kulevya. Bangi na muguka yatumika sana hapa Manda-Maweni na hawa vijana wadogo. Wazazi pia wametelekeza kabisa watoto wao hapa kutokana na hii pombe ya makore ambayo imegeuka kuwa donda sugu,” akasema Bw Ojuok.

Makore ni pombe ya kienyeji inayotengenezwa kutokana na wishwa, iwe ni wa nafaka kama vile mahindi, mtama au wimbi.

Wishwa huo huchanganywa na maji, hamira na sukari na kisha kuhifadhiwa pahala fulani kwa saa kadhaa ili ichachuke na kuwa kileo kikali.

Mara nyingine watengenezaji wa pombe hiyo hutumia kemikali kali na hatari ilmradi kileo kiwe kikali na chenye kulewesha haraka.

Katika kijiji cha Manda-Maweni, kikombe kimoja kikubwa cha pombe ya makore huuzwa kwa kati ya Sh25 na Sh30.

Mmoja wa walevi kijijini Manda-Maweni aliyehojiwa na Taifa Leo, lakini akasema tusimtaje, amesema yeye huhitaji vikombe vitatu pekee ndipo alewe kisawasawa.

“Wanaosema pombe ni mbaya wanakosea. Mlevi anayetumia ulevi wake vibaya ndiye wa kulaumiwa. Kwangu, makore ni pombe inayoniondolea msongo wa mawazo na kunisaidia kujiliwaza maishani. Nikibugia vikombe vitatu vya makore ninatosheka. Nalewa na kujikokota kuingia kwangu nyumbani kulala. Sina vita na mtu mimi,” akasema mlevi huyo.

Wakati huo huo, operesheni kali ya pombe haramu inaendelezwa kwenye vijiji vya Kibokoni na Mbuzi Wengi, tarafa ya Hindi, Kaunti ya Lamu.

Chifu wa Hindi, Jamal Keah mnamo Ijumaa ameongoza kikosi cha maafisa walioharibu vilabu vya pombe kwenye mitaa hiyo miwili inayotambulika kwa matatizo ya pombe haramu.

Mbali na pombe haramu, kijiji cha Kibokoni pia kinatambulika kwa ngono kupindukia, ambapo visa vya akina baba kushiriki ngono na mabinti zao wa kuwazaa vimeripotiwa mara kadhaa.

Hindi pia mara nyingi imetajwa mara kwa mara kuongoza katika visa vya unajisi wa wanawake, dhuluma za kingono kwa watoto na dhuluma za kijinsia kwa ujumla.

“Kwa miaka mingi tumekuwa na hili tatizo sugu la pombe haramu eneo hili. Twashukuru miaka ya hivi karibuni hilo tatizo limepungua kwani tunakabiliana nalo vilivyo. Akina baba, hasa mtaa wa Kibokoni, kwa sababu ya ulevi waliishia kushiriki ngono na mabinti zao. Juhudi zetu kupigana na pombe haramu zimechangia visa vya ulevi, ngono na dhuluma za kijinsia kupungua pakubwa siku za hivi karibuni. Hata leo nimeongoza maafisa wangu kumwaga pombe haramu eneo la Mbuzi Wengi na Kibokoni,” akasema Bw Keah.

Aliwasihi wananchi kuachana kabisa na ulevi wa pombe haramu na badala yake kuokoka.

“Ningeisihi jamii kubadili mienendo. Watu waanze kuingia misikitini na makanisani kwa ibada. Ikiwa mja anataka kunywa, basi heri anywe maziwa kuliko pombe,” akasema Bw Keah.

  • Tags

You can share this post!

Pasta Ezekiel Odero asema hana uhusiano wowote wa masuala...

Manamba wa matatu mashakani kwa kumuibia na kumbaka mwanamke

T L