• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:07 PM
Punda wagonjwa wachinjwa Gatundu nyama yao ikiingizwa jijini Nairobi

Punda wagonjwa wachinjwa Gatundu nyama yao ikiingizwa jijini Nairobi

NA MWANGI MUIRURI

KILO nyingine zaidi ya 3,000 za nyama ya punda zinakisiwa kupenyezwa katika soko la jiji la Nairobi baada ya wezi wa mifugo kuchinja punda wagonjwa katika Kaunti ya Kiambu.

Hii ni baada ya maafisa wa polisi wakiongozwa na Kamanda wa Kiambu Bw Perminus Kioi kupata vichwa, miguu na ngozi za punda katika kingo za mto wa Kariminu ulioko katika kijiji cha Karibaribi.

“Huu ni ushahidi kwamba kingo za mto huu zimegeuzwa kuwa kichinjio haramu cha wanyama walioibwa katika maboma ya wakulima eneo hili. Ni hali ya kututia wasiwasi kwa kuwa nyama hii inaingizwa katika soko jijini Nairobi,” akasema Bw Kioi.

Aliongeza kuwa baadhi ya punda hao waliochinjwa walikuwa na ugonjwa kulingana na ushahidi wazi ulioko katika ngozi zilizoachwa katika kichinjio hicho haramu.

“Kuna ngozi ambazo zinaonyesha maradhi ya uvimbe na vidonda. Baada ya punda kuchinjwa, nyama hupakiwa kwa magari na kisha kusafirishwa hadi sokoni. Ni hali ambayo inatushawishi tuwe makini sana kuhusu mitandao ya wizi wa mifugo katika soko la nyama,” akaongeza.

Katika msako huo wa Jumamosi asubuhi, hakuna mshukiwa aliyetiwa mbaroni, ikibainika kuwa habari za uvamizi wa maafisa hao ziliwafikia washirikishi wa uhalifu huo.

“Licha ya kwamba hatujamtia mbaroni yeyote, tuna uhakika kwamba maafisa watawanasa wote ambao wanaendesha njama hii ya kuwalisha wenzetu wa Nairobi nyama haramu. Tunataka kutoa wito kwa wateja wote wa nyama wawe makini sana hasa katika msimu huu wa sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya,” akatahadharisha.

Mnamo Novemba 14, 2023, kilo nyingine zaidi ya 2,000 ziliponyoka msako wa maafisa wa polisi katika Kaunti ya Murang’a na zikaingizwa jijini Nairobi.

Kwa mujibu wa Naibu Kamishna wa Murang’a Kusini Bw Gitonga Murungi, kilo 3,000 zilinaswa pamoja na matumbo ya kuandaa mutura.

“Sisi tulifanikiwa kunasa mshukiwa mmoja pamoja na gari moja la kusafirisha nyama hiyo. Katika mahojiano na mshukiwa, tulipata habari muhimu ambazo zimetuwezesha kuzima eneo hili kutumiwa kama ngome ya uchinjaji haramu wa mifugo,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Sababu ya waumini wa Akorino kuomba ‘mvua ya moto’...

Familia yaamini jeneza lililotupwa barabarani ni la mpendwa...

T L