• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 11:30 AM
Sababu ya waumini wa Akorino kuomba ‘mvua ya moto’ itembelee kilabu kimoja Ruiru

Sababu ya waumini wa Akorino kuomba ‘mvua ya moto’ itembelee kilabu kimoja Ruiru

NA MWANGI MUIRURI

Muungano wa wauminu wa dini ya Akorino nchini umetishia kulaani moto kilabu kimoja mjini Ruiru.

Hii ni kufuatia mtindo wa baa hiyo kuwapa wauminu wa dini hiyo nafasi ya kunengua viuno jukwaani na kisha kuchukua video zao na kuzipachika mitandaoni.

Katika mkanda huo wa video, watatu hao wanaonekana wakiwa wamepandwa na jazba huku wakijirusha na kunengua, wakiinama na kujipinda huku vijana nao waking’ang’ana kugusanagusana wakila densi.

Baadhi ya vijana hao pia ni wa dini hiyo ya Akorino, wakiwa na vilemba vichwani vya rangi za samawati na nyeupe hali ambayo imezua kejeli, shutuma na ucheshi mitandaoni.

Msemaji wa dini hiyo Bw Peter Karangu Muraya mnamo Ijumaa Disemba 1, 2023 aliongoza wasichana watatu kuomba msamaha baada ya kunaswa wakinengua mtindo wa bendover ndani ya baa hiyo alisema “tutawaombea mvua ya moto na biashara hiyo iishe”.

Wasichana hao ambao walijitambulisha kama Ciru wa miaka 21, Nyambura 19, na Mary aka Happy Gal wa miaka 21 walisema ni ibilisi wa ushawishi aliyewavamia na kuwafanya wahujumu imani yao.

Walisema kwamba wao walikuwa wamefika katika baa hiyo kuhudhuria hafla ya kusherehekea siku ya kuzaliwa kwa mmoja wao na katika ile hali ya raha, muziki kunoga na kujiachilia, wakajipata jukwaani.

“Sisi tunasemwa kwamba tulikuwa walevi lakini hatulewi. Tunasemwa kwamba tuko na akili punguani lakini tuko sawa. Wengine wanasema sisi ni makahaba lakini hawatoi ushahidi. Wanasema sisi ni mashetani lakini sisi ni binadamu tu ambao walikosea kidogo tu na tumeomba msamaha,” taarifa yao iliyosomwa na Happy Gal yasema.

Bw Muraya akiandamana na Bi Mary Esther wanjiku kwa jina maarufu la usanii likiwa ni Essy wa Willy walisema wamejitwika mzigo wa kuwasaidia watatu hao kukabiliana na mawimbi ya shutuma kufuatia mkanda huo wa video.

“Sisi hatulaumu watatu hawa ambao hata ni watoto. Hakuna kile wamefanya cha kutushinikiza kuwakashifu na kuwakana. Wamekubali walikosea na wameamua kuomba msamaha,” Bw Muraya akasema.

Aliongeza kuwa “tulicho na kinyongo nacho ni tabia ya baa hii kuwaalika waumini wetu na kisha kuwapa jukwaa la kuaibisha dini yetu”.

Alisema kwamba anajua kuna waumini ambao hata wakiwa na vilemba hulewa ndani ya baa hiyo.

“Watu kulewa ni uamuzi wao. Hao tutawafuata polepole ili tuwaagize wasiwe wanalewa wakiwa na vilemba vyetu kwa kuwa wanaifanya imani yetu kuonekana ikiwa ya walevi,” akasema.

Hata hivyo, alisema kuwanasa waumini hao wakiwa na vilemba huku wakilewa na kusakata densi kwa kutumia miondoko ya anasa ni kuingilia usiri wao na kuwaanika mitandaoni bila ya hiari yao ni kinyume na sheria.

“Ni kufuatia hali hiyo ambapo tunatoa onyo kwa mmiliki wa baa hii kwamba tutaandamana kama wasimamizi wa dini hii na tuombe Mungu aiteremshie laana ya mvua ya moto na iishe kabisa,” akasema.

Juhudi zetu za kuwasiliana na wasimamizi wa baa hiyo ziligonga mwamba, mwanamke aliyepokea simu akijifahamisha kama Alice akisema kwamba “kwa sasa hatuna maoni kuhusu kisa hicho”.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Kimeumana nyumbani kwa Neymar, mpenziwe aliyejifungua juzi...

Punda wagonjwa wachinjwa Gatundu nyama yao ikiingizwa...

T L