• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Familia yaamini jeneza lililotupwa barabarani ni la mpendwa wao aliyezikwa Septemba

Familia yaamini jeneza lililotupwa barabarani ni la mpendwa wao aliyezikwa Septemba

NA MERCY KOSKEI

WAKAZI wa kijiji cha Bagaria kilichoko eneobunge la Njoro katika Kaunti ya Nakuru wanaishi na wasiwasi baada ya kupata kipande cha jeneza kikiwa kimetupwa barabarani.

Wakazi hao kwa sasa wanaishi kwa hofu huku wakiamini jeneza hilo lililoondolewa katika kaburi lililofukuliwa na watu wasiojulikana, ni la Rose Njeri ambaye alizikwa Septemba alipoaga dunia baada ya kuugua saratani.

Mama huyo wa watoto wawili aliaga dunia mnamo Septemba 2023 akiwa na umri wa miaka 61.

Kaburi la marehemu Rose Njeri ambalo familia na wanakijiji wanashuku lilifukuliwa na jeneza kuondolewa. PICHA | MERCY KOSKEI

Alizikwa katika shamba lake la ekari tatu.

Kulingana na binti ya marehemu Bi Esther Wanjiru, aliondoka kuelekea shambani Jumanne asubuhi na dadake mkubwa walipogundua kuwa kaburi la mama yao lilikuwa limeharibiwa.

Anasema kuwa waliposogea karibu, walibaini kuwa watu wasiojulikana walikuwa wamehitilafiana na kaburi hilo, huku mchanga ukionyesha kuwa lilikuwa limechimbwa upya.

Aidha, hapo kulikuwa na alama za miguu.

Kulingana na Bi Wanjiru, baada ya kupumzisha mama yao, familia ilizingira kaburi hilo na uzio wa mbao lakini mbao zenyewe zilikuwa zimeondolewa na vipande kutupwa mita chache kutoka kwenye kaburi hilo.

“Huwa tunafika hapa kuangalia mazao yetu, lakini Jumanne tulibaini jambo lisilo la kawaida. Kaburi lilionekana kuwa limevurugwa. Tulishtuka tusijue la kufanya. Tulimwarifu shangazi ambaye alitushauri kuondoka na kutoa taarifa kwa chifu,” akaeleza Bi Wanjiru.

Aliongeza kwamba baada ya kumfahamisha chifu wa eneo hilo, aliwashauri kuripoti kisa hicho katika Kituo cha Polisi cha Naishi.

Hata hivyo, siku mbili baadaye, wakazi walipata vipande vya jeneza kando ya barabara, jambo ambalo liliipa familia wasiwasi na kuwaacha na maswali iwapo jamaa yao alifukuliwa na mwili kutupwa kwingineko.

Bi Esther Wanjiru, ambaye ni binti ya marehemu Rose Njeri akizungumza na wanahabari. PICHA | MERCY KOSKEI

Jioni sehemu nyingine ilipatikana mita chache karibu na mto.

Kulingana na Bi Wanjiru, mamake alinunua shamba hilo miaka michache iliyopita na kufichua kuwa hakuna mgogoro kwani wana hati miliki.

“Hatukulala usiku, hatujui ikiwa baada ya kufukua waliuchukua mwili huo na kuutupa mtoni au ikiwa tutaamka na kukuta mabaki ya mama yetu mlangoni au hata kando ya barabara,” alisema.

Dadake marehemu, Florence Wambui alisema kuwa aliarifiwa na mpwa wake kuwa kaburi la mama yao lilikuwa na dalili za kufukuliwa.

Bi Florence Wambui ambaye ni dadake marehemu Rose Njeri, akizungumza na wanahabari. PICHA | MERCY KOSKEI

Alisema kuwa aliwashauri watoe taarifa kwa Polisi hili waazishe uchunguzi.

Kulingana na Wambui, dadake amekuwa akiugua kwa miaka mingi.

Mnamo Aprili alikimbizwa katika Hospitali ya Kenyatta baada ya hali yake kuwa mbaya na kulazwa hospitalini kwa miezi sita.Alifariki Septemba 9,2023.

Alisema kuwa familia ililazimika kuweka hati miliki ili waruhusiwe kuchukua mwili baada ya kuacha biili kubwa ya matibabu.

‘Tuliumia roho alipoaga dunia, hata hivyo tulilazimika kumwacha apumzike baada ya kuugua kwa muda mrefu. Lakini sasa wamefungua kidonda hicho, hatuna amani kwani kaburi lake limechezewa. Hatujui ikiwa mabaki yake yapo au waliichukua,” alisema.

Familia hiyo ilisema kuwa wanatakiwa kutoa Sh75, 000 ili kupata agizo la mahakama kabla ya kufukuliwa ili kubaini ikiwa mwili huo uko.

Chifu wa eneo hilo Bw David Githiga alisema kuwa baada ya Bi Njoki kufariki, aliipatia familia hiyo kibali cha kuzika.

Chifu wa eneo la Bagaria Bw David Githiga akizungumza na wanahabari. PICHA | MERCY KOSKEI

Alisema kuwa mnamo Jumanne, familia ilimjulisha kuhusu matukio hayo na wanasubiri amri ya mahakama kabla ya kufukuliwa.

“Kwa kuwa hawakuupata mwili huo Jumanne, walishauriwa kusubiri uchunguzi. Lakini baada ya kupata sehemu ya jeneza, sasa maswali tele yameibuka. Hatujawahi kushuhudia kitu kama hiki, ni ajabu. Hakuna kitakachofanyika hadi amri ya mahakama itolewe,” alibainisha.

  • Tags

You can share this post!

Punda wagonjwa wachinjwa Gatundu nyama yao ikiingizwa...

Mto Tana wavunja kingo mafuriko yakitatiza shughuli za...

T L