• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 10:50 AM
Radol alenga kutinga anga za kimataifa katika uigizaji

Radol alenga kutinga anga za kimataifa katika uigizaji

Na JOHN KIMWERE 
ANAELEKEA kutinga miaka mitatu tangia aanze kujituma kwenye masuala ya maigizo ambapo amepania kufikia hadhi ya filamu za Hollywood miaka ijayo.
Aidha ni miongoni mwa mabinti wanaoendelea kuvumisha jukwaa la uigizaji nchini. Eleyne Mutsoli maarufu Radol anasema kuwa amepania kujituma mithili ya mchwa kuhakikisha anatinga upeo wa kimataifa kama Angelina Jolie mzawa wa Marekani, aliyeshiriki filamu kali kama Magnificent.
Kisura huyu aliye pia mpondoaji (Makeup Artist) amehitimu kwa shahada ya digrii katika masuala ya uigizaji kwenye Chuo Kikuu cha Multimedia (MMU). ”Ndio ninakuja katika masuala ya maigizo lakini ninaamini ninatosha mboga ambapo ninatamani kujituma kiume kuhakikisha nimetinga hadhi ya juu,” alisema.
MPASUAJI
Anasema kuwa akiwa darasa la sita alisoma kitabu cha mwandishi Ben Carson kiitwacho ‘Gifted Hands’ ambapo alipata motisha kuwa mpasuaji. ”Licha ya hayo taaluma yangu ya uigizaji ilianza kuchipuka nilipotinga kidato cha tatu ambapo nilitamani kusomea masuala ya burudani hadi Chuo Kikuu,” binti huyu anasema na kuongeza kuwa anatamani kuwa balozi wa Kenya kwa kutangaza utamaduni wa taifa hili kama ilivyo nchini Nigeria na Ghana.
Ingawa ni miaka michache tangu ajiunge na uigizaji binti huyu aliyezaliwa mwaka 1996 anajivunia kushiriki filamu nyingi tu ikiwamo, Kortini (Ebru TV), Kina (Maisha Magic Plus), Varshita (Maisha magic East) na  Aunty Boss (NTV) kati ya zingine.
Eleyne Mutsoli maarufu Radol…Picha/JOHN KIMWERE
”Kando na kazi hizo pia chuoni tulishiriki filamu ‘A cry for help,’ na ‘Tears of Fury’, ambazo hadi leo zimenifanya nihisi nikiwa mshindi. Amepania kuwa kati ya waigizaji waliopiga hatua ndani ya miaka mitano ijayo.
‘Katika kipindi hicho nataka kuwa na kampuni yangu pia niwe nimezalisha filamu inayoangazia utamaduni wetu. ”Anatoa wito kwa serikali za Kaunti zote 47 zijenge na kufungua kumbi za burudani kwa ajili ya wasanii wanaoibukia kuonyesha vipaji vyao.
Pia anasema itakuwa bora endapo Wakenya watajifunza kutokana na mataifa yanayoendelea ambapo wasanii wamejitwika jukumu la kutangaza utamaduni wao kupitia uigizaji. Kwa waigizaji wa kimataifa anasema angependa kufanya kazi na Genevive Nnaji wa Nigeria aliyeshiriki filamu nyingi tu ikiwamo Blood Sisters kati ya zingine.
Pia ansema angependa  kushirikiana na Mkenya mwenzake anayetamba katika filamu za kimataifa, Lupita Nyong’o aliyetwaa tuzo kutokana na filamu yake 12 Years A slave  na pia Black Panther.
”Katika mpango mzima hapa nchini hauwezi kukosa kumtaja  mwigizaji mahiri, Sarah Hassan aliyeshiriki filamu iitwayo, Plan B pia Crime Justice,” akasema. Kuhusu mahusiano dada huyu anasema kwa sasa hana mpenzi lakini yupo tayari kuanzisha na yeyote atakayeona anamfaa.
Anasema mapenzi sio jambo la kukimbilia ni rahisi kupoteza mwelekeo maishani. Kwa waigizaji wanaokuja kwenye gemu anawashauri kuwa kamwe wasiwe na pupa maana jukwaa ya maigizo sio mteremko.
  • Tags

You can share this post!

LEONARD ONYANGO: Siku ya Utamaduni ilifaa kuadhimishwa...

Msanii alisha asema usaliti, vurugu zilimtoa machozi

T L