• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Raila, Kalonzo wapeleka vita vyao Mt Kenya

Raila, Kalonzo wapeleka vita vyao Mt Kenya

Na BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa chama cha ODM Raila Odinga na mwenzake wa Wiper Kalonzo Musyoka wameanza kunyemelea eneo la Mlima Kenya kutafuta uungwaji mkono huku tofauti kati yao zikionekana kupanuka.

Mwishoni mwa wiki, Bw Musyoka alikuwa katika Kaunti ya Murang’a kwenye ziara iliyofanikishwa na aliyekuwa katibu wa wizara, Bw Irungu Nyakera ambapo alisisitiza kuwa jina lake litakuwa kwenye debe katika uchaguzi mkuu ujao.

Mnamo Jumatatu, naye Bw Odinga alizuru Kaunti ya Kiambu. Bw Musyoka ambaye aliepuka kuandamana na viongozi wa eneo hilo waliochaguliwa katikas, alihutubia wakazi wa wadi za Ithanga, Kakuzi, Makuyu na Kambiti. Alitumia ziara hiyo kumjibu Bw Odinga aliyemlaumu kwa kusema hatamuunga mkono kwenye uchaguzi mkuu ujao.

“Nitaendelea kubweka hadi viongozi wajue kuheshimu mikataba yoyote wanayofanya mbele ya umma au kwa siri. Ni lazima kuwe na uadilifu katika siasa na viongozi wanafaa kuheshimu ahadi bila kuziruka,” alisema Bw Musyoka.Akiwa Mombasa mnamo Alhamisi wiki jana, Bw Odinga alimkashifu Bw Musyoka kwa kudai hatamuunga mkono ilhali hajatangaza kugombea urais 2022.

Bw Musyoka alisema kwamba ataungana na Jubilee iwapo chama hicho kitakubali “muungano wa kisiasa usio na ujanja” lakini akakasisitiza kwamba hatakuwa mgombea mwenza wa Bw Odinga.Mnamo Jumatatu, Bw Odinga alitembelea Kaunti ya Kiambu alikohutubia wafanyabiashara kwa mwaliko wa aliyekuwa naibu gavana wa Kaunti ya Nairobi, Bw Polycarp Igathe.

Bw Odinga ambaye amekuwa akiunga maamuzi ya serikali ya Jubilee tangu handisheki na Rais Kenyatta mnamo Machi 9, 2018, alisema viwango vya juu vya ushuru vimelemaza biashara ndogo na kuua motisha ya Wakenya katika biashara.

Katika hatua iliyolenga kuliwaza eneo la Mlima Kenya ambako wafanyabiashara wengi wanatoka, Bw Odinga alisema viwango vya juu vya ushuru vimefanya biashara nyingi kufungwa na watu wengi kupoteza kazi.Kulingana na wadadisi wa siasa, kauli ya Bw Odinga ambaye amekuwa akiunga serikali ikiongeza ushuru wa bidhaa muhimu, inalenga kumtafutia uungwaji mkono wa wakazi wa eneo hilo ambao wamekasirishwa na serikali kwa kuua biashara zao.

“Alikuwa akihutubia wafanyabiashara na kama mwanasiasa anayefahamu kufurahisha watu aliwaambia walichotaka kusikia ikizingatiwa kuwa uchaguzi mkuu unakaribia. Analenga kujitakasa na maovu ya Jubilee ambayo amekuwa akiunga mkono kwa miaka mitatu ikifanya maamuzi yaliyovunja matumaini ya watu wengi,” alisema mchanganuzi wa siasa Hyslop Waikwa.

Naibu Rais William Ruto ambaye wachanganuzi wa siasa wanasema ndiye mpinzani mkuu wa Bw Odinga kwenye uchaguzi mkuu ujao amekuwa akilenga wafanyabiashara wadogo katika kampeni yake ya hasla.Ametumia kampeni hiyo kupenya eneo la Mlima Kenya akiahidi mfumo wa uchumi utakaoimarisha maisha ya wafanyabiashara wadogo iwapo atashinda urais.

Bw Waikwa anasema Bw Odinga na Bw Musyoka wanang’ang’ania kuungwa mkono na Rais Kenyatta na ziara zao wakati wametofautiana zinaashiria kuwa kila mmoja anataka kuonyesha ndiye anayekubalika eneo hilo la Mlima Kenya.

Kwenye ziara yake Kiambu, Bw Odinga aliandamana na Seneta wa Siaya James Orengo, aliyekuwa mbunge wa Gatanga, Bw Peter Kenneth na mbunge wa kuteuliwa miongoni mwa wengine. Wandani wa Bw Musyoka na Bw Odinga wanasema viongozi hao wana haki ya kutembelea eneo lolote Kenya kuzungumza na watu.

  • Tags

You can share this post!

Heko Facebook kuzima akaunti za chuki Ethiopia

Somalia, Afghanistan hatari zaidi kwa maisha ya watoto