• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Ratiba ya mazishi ya Nyachae yabadilishwa

Ratiba ya mazishi ya Nyachae yabadilishwa

Na WYCLIFFE NYABERI

WAKAZI wa kaunti ya Kisii wametoa hisia mseto kuhusu kubadilishwa kwa ratiba ya mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Nyaribari Chache na waziri katika serikali zilizopita, Simeon Nyachae.

Awali, ibada hiyo ilipangwa kufanyika katika uwanja wa michezo wa Nyanturago, lakini kamati andalizi ikabatilisha uamuzi huo dakika za mwisho. Sasa itaandaliwa katika uwanja wa michezo wa Gusii, maarufu kama uwanja wa Nyantika Maiyoro.

Kulingana na mmoja wa waandalizi na rafiki wa karibu wa familia ya marehemu mzee Nyachae, Bw Steve Arika, uamuzi wa kubadilisha uwanja wa Nyanturago uliafikiwa baada ya kubainika kuwa uwanja huo haungepokea halaiki kubwa ya waombolezaji ambao wanatarajiwa kuhudhuria mazishi ya kiongozi huyo Jumatatu.

“Baada ya mashauriano ya kina kati ya familia, serikali na kamati andalizi, ilibainika uwanja wa Nyanturago ni mdogo na hatungepata sehemu ya kuyaegesha magari. Hivyo basi, iliamuliwa mazishi hayo yapelekwe uwanja wa Gusii ndiposa waombolezaji wapate nafasi murwa ya kuomboleza aliyekuwa kiongozi wetu,” akasema Bw Arika.

Pindi tu wakazi wa Nyanturago walipopokea habari hizo Alhamisi jioni, walilalama kuhusu uamuzi huo huku wakidokeza kwamba uwanja wao ndio uliokuwa unapendwa na kuenziwa na Mzee Nyachae alipokuwa hai.

“Hii ni kuenda kinyume na jinsi mzee wetu alivyotaka. Akiwa mjumbe wetu, alikuwa akifanya sherehe zote za kitamaduni hapa na hatua ya kupeleka mazishi yake mjini Kisii haijatufurahisha,” akasema Bw Alloys Moindi, mkazi wa Nyanturago.

Wenyeji wa Nyanturago walitamaushwa na uamuzi huo, wahudumu wa bodaboda mjini Kisii wamefurahia hatua ya kuleta sherehe hizo katika uga wa michezo wa Gusii.

  • Tags

You can share this post!

Kanu, Jubilee walaumiana kuhusu fujo

Mchuano wa mkondo wa pili wa Europa League kati ya Arsenal...