• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Rotich atabasamu DPP akikataa kuhoji mashahidi kesi ya Sh63 bilioni

Rotich atabasamu DPP akikataa kuhoji mashahidi kesi ya Sh63 bilioni

NA RICHARD MUNGUTI

KESI ya madai ya ubadhirifu wa Sh63 bilioni dhidi ya aliyekuwa waziri wa Fedha Henry Rotich kuhusiana na mabwawa ya Arror na Kimwarer imeendelea kubomoka huku Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) jana akikataa kuwahoji mashahidi saba.

Idadi ya mashahidi ambao DPP amekataa kuwahoji imetimia 13.

Wiki iliyopita aliyekuwa Waziri wa Kilimo Peter Munya alifika kortini lakini DPP kupitia wakili Geoffrey Obiri akasema “hatuna swali kwa shahidi huyu.”

Mawakili wa Serikali Bw Obiri na Oliver Mureithi jana walimweleza Hakimu Mkuu wa mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Bi Eunice Nyuttu kwamba hawana chochote cha kuwauliza mashahidi hao.

Mashahidi aliokataa kuwahoji Bw Obiri ni William Otieno Ogolla, Samuel Kosgey, Mwenda Wanjohi, Anne Wambui Macharia, Boniface Mamboleo, Festus Kivisu, Maina Kiondo, Benedict Omondi na Kimani Kiiru.

Mashahidi hao walikuwa wameagizwa wakamatwe walipokosa kufika kortini.

Lakini walipofika kortini waliomba msamaha.

Baada ya kuwaapishwa Bw Obiri alisema, “sina maswali kwa hawa mashahidi.”

Aliposema hayo Bi Nyuttu aliwaruhusu mashahidi kuondoka mahakamani.

Ikumbukwe kwamba Jumatatu Septemba 11, 2023  Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma aliwasilisha ombi akitaka hakimu Eunice Nyuttu anayesikiza kesi dhidi ya aliyekuwa Waziri wa Fedha Henry Rotich ya ubadhirifu wa Sh63 bilioni za ujenzi wa mabwawa hayo ya Arrow na Kimwarer, ajiondoe katika kesi hiyo akidai hatendi haki.

Hata hivyo, hakimu huyo alimwamuru kiongozi wa mashtaka Geoffrey Obiri awasilishe ombi rasmi ndipo mawakili wa washtakiwa wajibu.

Kumekuwa na maswali kuhusu mwelekeo wa kesi hiyo haswa katika uitaji wa mashahidi ambao baadhi yao wamelazimika kushurutishwa kujitokeza kiasi cha kupewa ilani ya kukamatwa iwapo watakataa kufika mahakamani.

Kisa cha punde zaidi kilikuwa wiki chache zilizopita ambapo aliyekuwa Waziri wa Kilimo Peter Munya aliamriwa kufika kutoa ushahidi kama mmoja wa wafichuzi wa wizi wa pesa hizo za mabwawa, kama inavyodaiwa.

Na alipowasilishwa kortini, wala hakuulizwa maswali na ikabidi kurejea nyumbani.

Mahakama ililazimika kutoa ilani ya kukamatwa kwa wafanyakazi wanne wa umma ambao wameorodheshwa kama mashahidi, wakitakiwa kufika mahakamani kuulizwa maswali.

  • Tags

You can share this post!

Wakazi wa Taita Taveta wataka Ruto atimize ahadi alizowapa

Mwanamke ateketea na kubaki majivu katika mkasa wa moto...

T L