• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:15 PM
Ruto ateua Isaac Melly kuwa kamishna wa SRC

Ruto ateua Isaac Melly kuwa kamishna wa SRC

NA CHARLES WASONGA

RAIS William Ruto amempendekeza aliyekuwa Seneta wa Uasin Gishu Isaac Melly kuwa Kamishna wa Tume ya Kukadiria Mishahara na Marupurupu ya Watumishi wa Umma (SRC).

Jina la Melly sasa limewasilishwa kwa Kamati ya Bunge kuhusu Fedha, inayoongozwa na Mbunge wa Molo Kuria Kimani, ambayo itampiga msasa kubaini ufaafu wake. Ikiwa kamati hiyo na kamati ya bunge lote litaidhinisha uteuzi wake, Rais Ruto atamteua Bw Melly rasmi kuwakilisha Tume ya Huduma za Bunge (PSC) katika SRC.

“Ningependa kuwasilisha ujumbe kutoka kwa Rais kuhusiana na uteuzi wa mwakilishi wa Tume ya Huduma za Bunge katika tume ya kukadiria mishahara na marupurupu ya watumishi wa afya (SRC),” Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula akasema kwenye taarifa yake kwa wabunge Jumanne alasiri.

Rais Ruto amempendekeza Melly kuwa kamishna wa SRC kulinganana mamlaka aliyonayo kwa mujibu wa kipengele cha 230 cha Katiba na Sheria ya SRC ya 2011.

“Kwa hivyo, Rais sasa anaitaka bunge hili kuidhinisha jina la Bw Melly kuwa kamishna wa SRC,” Bw Wetang’ula akasema.

Bw Melly ni miongoni mwa watu 10 ambao PSC iliwaorodhesha kwa uteuzi katika nafasi hiyo.

Wengine ni wabunge wa zamani Naomi Shaban (Taveta), Florence Mutua (Mbunge Mwakilishi wa Busia), David Were (Matungu), Peter Mwathi (Limuru) na Jimmy Angwenyi (Kitutu Chache Kaskazini).

Mahojiano kwa ajili ya nafasi hiyo yalifanyika Machi 22, 2023

Wakati huu SRC inaongozwa na Bi Lyn Mengich kama mwenyekiti huku Amani Komora akiwa naibu mwenyekiti.

Inayo makamishna wanane huku Anne Gitau ni Afisa Mkuu Mtendaji.

  • Tags

You can share this post!

Olunga aongoza vita vya kuwa mfungaji bora Al Duhail...

CJ Koome aonya wanaonyemelea na kunajisi watoto

T L