• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 5:50 AM
Seli kwa kusimika bendera ya Somalia

Seli kwa kusimika bendera ya Somalia

BRIAN OCHARO na KALUME KAZUNGU

WANAUME sita waliokamatwa kwa madai ya kushiriki ugaidi wataendelea kuzuiliwa kwa siku 15 ili kuwapa polisi muda wa kukamilisha uchunguzi wao, Mahakama ya Mombasa imeamua.

Kulingana na ripoti za polisi, watu hao ambao uraia wao hautambuliwa walikamatwa katika ufuo wa bahari wa Nyali Sun Africa wakipeperusha bendera ya Somalia huku wakiimba nyimbo za Kisomali mnamo Jumamosi.

Walitambuliwa kama Ridhman Issack, Jamal Abdi, Mohammed Bare, Abdimalik Noor, Abdiraffi Sheikh na Saad Ibrahim Salat.

Katika hati ya kiapo, Koplo Gideon Wambua aliarifu korti kwamba sita hao wanachunguzwa kwa madai ya kuwa wanachama wa kundi la kigaidi.

Washukiwa hao sita walifikishwa kortini jana mbele ya Hakimu Mwandamizi Mkazi, Rita Amwayi.

Wapelelezi wanasema wanataka kufahamu nia ya washukiwa ya kusimika bendera ya kigeni nchini, na kwa nini walichagua sehemu ya umma kufanya sherehe zao.

Bw Wambua alisema kitengo cha Polisi wa Kupambana na Ugaidi (ATPU) kimeandikia idara ya kitaifa ya usajili ili kuthibitisha ikiwa vitambulisho walivyopatikana navyo ni halali.

“Tumepeleka simu za mkononi za washukiwa katika makao makuu ya ATPU kwa uchambuzi zaidi,” afisa huyo akaongeza kusema.

Kwingineko, maswali yameibuka baada ya kubainika kuwa mpango wa serikali kuwapa wavuvi wa Kaunti ya Lamu vitambulisho maalumu vya kidijitali haujatekelezwa miaka mitatu baada ya kuzinduliwa.

Kadi hiyo inayofahamika kama ‘Mvuvi Card’ ilinuiwa kusaidia kuzuia magaidi kuingia katika bahari za Kenya wakijifanya kuwa ni wavuvi.

“Walitushirikisha kwenye mpango huo. Tukaukaribisha kwa mikono miwili. Walitupiga picha. Pia walichukua majina yetu, nambari za vitamblisho na maelezo mengine waliyotaka kujumuisha kwenye kadi hiyo. Kilichosalia ilikuwa ni kungoja kadi. Tunashangaa kwamba miaka inasonga na hakuna aliyepewa kadi hiyo maalum. Serikali itujulishe ikiwa mpango huo bado upo ama waliukatiza,” akasema Mwenyekiti wa Vyama vya Ushirika wa Wavuvi (BMU) tawi la Lamu, Mohamed Somo.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Irungu Macharia alikiri kwamba mpango huo haujatekelezwa lakini akataka wavuvi wawe na subira.

“Kumekuwa na changamoto za kiufundi katika kuandaa vitambulisho hivyo. Tuko kwenye harakati za kutatua changamoto hiyo. Wavuvi wasiwe na shaka. Wajue mpango bado upo,” akasema Bw Macharia.

  • Tags

You can share this post!

Vigogo wapigania Karua kuunda muungano naye

Uswisi wadengua vigogo Ufaransa na kujikatia tiketi ya...